YANGA RAAAHA

Penati ya Ngoma yaota mbawa L Tambwe, Simon Msuva wang’ara Simba yachezewa sharubu Mbeya

BURUDANI - - MBELE - NA NASRA KITANA

YANGA kweli raha isiyo na kifani, kwani jana imeendeleza wimbi la ushindi kwa kuinyuka Toto African mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara, uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pambano hilo, lilianza kwa kasi, Yanga nusura waandika bao dakika ya kwanza kupitia kwa Amis Tambwe, baada ya kupokea pande safi la Juma Abdul.

Thabit Kamusoko naye, dakika ya sita alishindwa kuiandikia Yanga bao, baada ya shuti alilopiga kushindwa kulenga goli.

Dakika moja baadae, Ali Mustapha ‘Barthez’ chupuchupu afungwe kama Japhet Vedastus wa Toto angekuwa makini. Barthez alitoka vibaya golini kwake, lakini mchezaji huyo wa Toto alishindwa kutumia makosa ya kipa wa Yanga.

Baada ya Yanga kukoswa, waliwageuzia kibao wapinzani wao na dakika ya nane, Abdul aliipatia timu yake bao la kuongoza alipopiga shuti akiwa umbali wa mita 18.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwafanya Yanga wazidi kuliandama lango la Toto, dakika ya 30 Donald Ngoma aliikosesha timu yake bao baada ya shuti lake kuishia mikononi mwa kipa Mussa Kilungi.

Iliposalia dakika moja kuwa mapumziko, Mwamuzi Ahmada Simba wa Kagera, aliwapa Yanga penati baada ya Calos Protas kuunawa mpira eneo la hatari, lakini Ngoma alikosa.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kumuingiza Simon Msuva aliyechukua nafasi ya Abdul na mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 48.

Msuva alifunga bao la pili baada ya kuwatoka walinzi wa Toto na kuachia mkwaju lililojaa kimiani.

Toto walipata bao lao dakika ya 55 kupitia kwa Miraji Athumani, akifunga kwa kichwa kufuatia shuti la adhabu ndogo lililopigwa na Salmin Hoza.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwaongezea Toto morari kuliandama lango la Yanga wakiwa na lengo la kusawazisha ili wagawane pointi na vinara hao wa ligi kuu.

Ili kuongeza nguvu zaidi, Yanga waliwaingiza Andrey Coutinho na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuchukua nafasi za Kelvin Yondan na Godfrey Mwashiuya.

Toto nao walimuingiza William Kimanzi kuchukua nafasi ya Hoza, Jafari Mohammed nae badala ya Japhet Vedastus.

Bao la tatu la Yanga, liliwekwa kimiani na Tambwe, akimalizia kazi nzuri ya Msuva kabla ya Msuva kufunga la nne dakika ya 90 akiunganisha pande la Coutinho.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu kutoka Mbeya anaripoti kuwa, Simba jana ilivutwa mkia kwa kufungwa bao 1-0 na Prisons katika mchezo uliopigwa uwanja wa Sokoine.

Yanga: Ali Mustapha ‘Barthez,’ Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Vincent Bosou, Thabit Kamusoko, Malimi Busungu, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amis Tambwe na Godfrey Mwashiuya.

Toto: Mussa Kilungi Hassan Khatib, Robert Magadula, Hamis Kasonga, Carlos Protas, Salmin Hoza, Japhet Vedastus, Abdallah Seseme, Everigestus Bernard, Edward Christopher na Miraji Madenge.

CAROLS Protas (kushoto) na Salimin Hoza wa Toto African wakichuana na Haroun Niyonzima wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana. Yanga ilishinda mabao 4-1. (Picha na Emmanuel Ndege).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.