BISKUTI YAZUA KIZAZAA

BURUDANI - - WAZO | HOJA -

DADA aliyekuwa akisubiri ndege ya kuunganisha alichuma dhambi baada ya kumshambulia kwa matusi mtu ambaye hakumkosea chochote.

Mrembo huyo akiwa anasubiri ndege uwanjani hapo, mara wakatangaziwa muda wa kusubiri utakuwa saa 2.

Tangazo hilo likamsukuma aende kununua gazeti na biskuti na kurudi kukaa sehemu ya abiria wanaosubiri kusafiri ambapo alipokaa pia alikuwepo kijana ambaye pia alikuwa msafiri.

Ghafla dada alishangaa alipokuwa akitoa biskuti kwenye boksi aliloweka pembeni yule kaka anachukua moja na kuendelea kula hadi mwanamke akamkata jicho kutaka kumtukani lakini alijizuia na muda wote yule kaka alikuwa anatabasamu.

Waliendelea hivyo hadi ikabakia biskuti moja ambayo kijana akawahi kuichukua akaimega nusu akampa huyo dada, ambaye alinyanyuka kwa ghadhabu na kuanza kumdhalilisha huyo kwa kuvamia vitu vya watu badala ya kununua vyake.

Licha ya kudhalilishwa jamaa hakujibu mara walitangaziwa muda wa kuingia kwenye ndege, dada akapanda na kumuacha huyo kaka anasubiri ndege nyingine.

Baada ya mrembo kukaa kwenye kiti chake alifungua mkoba ili aweke simu yake, mara alishtuka kuona boksi lake la biskuti zima halijafunguliwa kumbe muda wote aliokuwa mkali kama pilipili alikuwa anakula biskuti za kaka aliyemuacha uwanja wa ndege.

Alijuta sana akatokwa machozi kwa jinsi alivyomdhalilisha yule kaka na muda wa kurudi kuomba msamaha haukuwepo tena kwani milango ya ndege ilishafungwa na kuanza kuondoka ikivuta kasi ya kupaa...!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.