YANGA YATIMUA WAGENI

Masikini Mwashuiya!

BURUDANI - - MBELE - NA SOPHIA ASHERY

KAMA kuna mchezaji wa kigeni mwenye ndoto za kutua Yanga na kumwaga wino kwa ajili ya msimu ujao asijimbue kufanya hivyo, baada ya klabu hiyo kutangaza haihitaji tena vifaa vya kutoka nje ya nchi.

Mkakati uliobaki Jangwani kwa sasa ni kusajili wachezaji wazawa wenye uwezo wa kucheza na kushindania namba na waliopo.

Akizungumza na BURUDANI jana Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema zaidi ya wachezaji watano ambao si Watanzania walikwenda Jangwani kuomba kufanya majaribio katika timu yake, lakini walikataliwa.

Alizitaja nchi wanazotoka wachezaji hao kuwa ni zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Kenya na kusema hawakupata nafasi ya kujaribiwa kwa kuwa Yanga wakati huu hawahitaji mchezaji yeyote wa kimataifa.

Hafidh alisema hawahitaji kufanya usajili wa wachezaji wa kimataifa kwa kuwa hawana nafasi ya kujaza.

Alisema wachezaji wa kimataifa waliopo katika kikosi chake wana mikataba itakayomalizika msimu ujao na wana uwezo wa kucheza katika timu yake hivyo hawana haja ya kufanya usajili.

Hafidh alisema usajili unaofanyika kwa sasa wa wachezaji wa ndani na kusema Kamati ya Usajili inaendelea na taratibu za kusajili wachezaji ambao wataisaidia timu yake.

“Unajua sisi tupo katika mashindano tofauti na timu nyingine kama Simba na Azam FC ambazo kwa wakati huu zenyewe zinajiandaa na msimu mpya lakini tunaendelea na michuano hivyo si vyema kuanza kuhangaika kupangua timu,” alisema Hafidh.

Wachezaji wa kimataifa waliopo katika timu ya Yanga ni Obren Chirwa (Zambia), Donald Ngoma, Thaban Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda) na Mbuyu Twite (DRC).

Wakati huo huo kiungo wa pembeni Geoffrey Mwashuiya atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu kutokana na kuumia goti katika mechi dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.

Mchezaji huyo ameumia goti la kushoto.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.