Mawakala wanaovuna fedha

Zinawafuata wakiwa wamekaa miguu juu

BURUDANI - - MBELE -

LONDON, England JOTO la usajili limeanza kupamba moto, lakini wakati klabu zikipigana vikumbo kugombea wachezaji, kando kuna mawakala watano waliotulia tuli kwenye viti vyao wanasubiri fedha ziingie tu.

Mawakala hao watano ndio ambao kwa sasa wameishika dunia na wanasubiri wasikie ‘dili’ zimekamilika, wao watie chao mfukoni. JORGE MENDES

Ni mfalme wa mawakala, Mendes mpaka sasa anakadiriwa kuwa amevuna utajiri usiopungua dola bilioni 1 kutokana na mikataba minono iliyomuingizia pesa na ambayo inaendelea kumfaidisha, kutokana kuwamiliki wachezaji James Rodriguez, Angel Di Maria, Diego Costa na Cristiano Ronaldo kwenye orodha yake.

Ronaldo ana uhusiano wa pekee na Mendes, ambapo nyota huyo wa Ureno alikuwa mpambe wa Mendes alivyofunga ndoa mwaka jana.

Mendes amepiga pesa ndefu kutoka Manchester United kwa miaka kadhaa ya hivi karibuni, amechota euro milioni 24 kutoka kwa Mashetani Wekundu mwaka 2014 pekee.

Kocha Sir Alex Ferguson alimpigia saluti wakala huyo mwenye umri wa miaka 50 akionyesha kumkubali baada ya kumzungumzia kwenye kitabu chake kinachoitwa ‘Leading’, aliposema: “Kuna baadhi ya mawakala wenye heshima, lakini huhitaji kuhesabu vidole vyote vya mkono kumtaja. Mmojawapo ni Jorge Mendes.”

Wakala huyo katika majira haya ya kiangazi amevuta mkwanja kutoka kwa: Jose Mourinho, Renato Sanches, Angel Gomes, William Carvalho, James Rodriguez na Diego Costa. MINO RAIOLA

Mino ametuliza miguu yake tulii chini ya meza baada ya kuweka chake mfukoni kutoka Old Trafford, ambapo amewauza Zlatan Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan kwa kocha Jose Mourinho.

Raiola atapiga pesa nyingi kutoka Man United kama wakimalizana kuhusu Paul Pogba anayetajwa kurejea tena kwa Mashetani Wekundu.

Gazeti la Sunday Times linadai wakala huyo huenda akavuna pauni milioni 25 kutoka kwa Pogba pekee mbali ya wachezaji ambao ameshawauza katika klabu hiyo ya England.

Sir Ferguson alitupa lawama kwa Raiola kutokana na Pogba kuondoka Man United mwaka 2012, ingawa wakala huyo Mtaliano mzaliwa wa Uholanzi hakujali chochote juu ya alivyokuwa anafikiriwa kuhusu hilo.

Raiola aliendelea kupiga dili za mauzo ya wachezaji na kwa mujibu wa jarida la Forbes, mwaka jana alishiriki kwenye mikataba yenye thamani ya pauni milioni 186.

Mwanzo wa mkutano wake na Ibrahimovic, alimwambia nyota huyo wa Sweden aende anapopataka. Zlatan sasa anamwelezea Raiola kama wakala, rafiki na mshauri wake.

Amepata ‘chajuu’kutoka kwa: Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan, Paul Pogba, Romelu Lukaku, Blaise Matuidi na Mario Balotelli. JONATHAN BARNETT

Ni wakala Muingereza anayesubiri kuingiza fedha nyingi katika muda mfupi sana, japo sio kwenye dili hizi za uhamisho.

Barnett mwenye umri wa miaka 66 ni wakala anayemiliki kampuni ya Stellar Group, ambayo inashikilia orodha ya wachezaji soka watapao 150 duniani.

Aliongoza majadiliano ya uhamisho ulioweka rekodi duniani wa Gareth Bale kwenda Real Madrid pamoja na Luke Shaw aliyenunuliwa kwa pauni milioni 30 na Manchester United msimu uliofuata.

Lakini kama ilivyo kwa wachezaji na klabu nyingi, Barnett binafsi, amevutiwa na faida aliyopata China msimu ulioisha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters katika taarifa yake ya Mei mwaka huu, kampuni nne za uwekezaji za China ziliwasilisha maombi yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 140 kwa Stellar Group.

Amefaidika kwa mauzo ya Grzegorz Krychowiak na Wojciech Szczesny. VOLKER STRUTH

Mjerumani huyu ni wakala mwenye ushawishi mkubwa kwenye ligi ya Bundesliga, lakini Struth amempoteza mmoja wa wateja wake muhimu msimu huu.

Mario Gotze alijitoa katika kampuni ya SportsTotal mwisho wa msimu uliopita, wakati hatima yake ya baadaye ikiwa haijulikani anaenda wapi.

Mchezaji huyo aliamua kubaki Bayern Munich, licha ya klabu hiyo kuweka wazi kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 hakuwa sehemu ya mipango yao.

Wakati hatima yake ikiwa haijawekwa wazi, Gotze aliamua kwamba maslahi yake bora yalindwe na ndugu zake, kuliko Volke, ambaye mwaka uliopita ‘alimtumbua’ kocha Pep Guardiola akimtuhumu kumuangamiza mteja wake.

Volke na kampuni yake ya SportsTotal bado wamepiga pesa katika vitabu vya kumbukumbu zao za mauzo ya wachezaji.

Iliwauza: Toni Kroos, Omer Toprak na Timo Horn. CONSTANTIN DUMITRASCU

Dumitrascu kampuni yake ya Mondial Sports Management iliipiku kampuni ya Gestifute ya Mendes iliyopata euro milioni 61 mwaka jana, huku yenyewe ikilipwa kamisheni ya euro milioni 910 kutokana na uhamisho uliowahusisha Anthony Martial, Douglas Costa, Yohan Cabaye, Dimitri Payet na Aleksandar Mitrovic.

N’Golo Kante pia ameipa faida kampuni ya Mondial alipojiunga na klabu ya Leicester mwaka jana kwa kuipa ‘kamesheni’ ambayo ni sawa na waliyopata kutoka kwa kiungo huyo ya pauni milioni 32 kwa uhamisho wake kwenda Chelsea mwisho wa wiki iliyopita.

Hana tabia kama za mawakala wengine, Dumitrascu mtulivu, anatazama biashara na kufuatilia ustawi wa wateja wake.

Akiwa anaendesha shughuli zake Frankfurt, mwaka huu anatarajiwa kuwa tishio kwa kupata dili nono kama wachezaji waliopo kwenye orodha yake wakipata soko.

Wachezaji ambao kwake ni miraji ya pesa ni: Samuel Umtiti, Edinson Cavani, Nemanja Matic, Axel Witsel, Raphael Varane, Olivier Giroud, Geoffry Kondogbia, Aymeric Laporte, Moussa Sissoko, Dimitri Payet na Felipe Anderson.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.