Jose Omog abwagiwa zigo, Yanga yaivaa TFF

BURUDANI - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

WAKATI klabu ya Yanga imeomba ratiba ya ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao isogezwe mbele kwa madai kuwa imewabana, Simba wamesema mwenye kujua hilo ni kocha wao Joseph Omog.

Akizungumza na gazeti hili Katibu Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Kahemele alisema kuwa suala la ratiba na mapungufu yake litajadiliwa na Kamati ya Ufundi chini ya kocha wao.

“Mimi binafsi sina maoni yoyote kuhusiana na hiyo ratiba kwa sababu hainihusu, labda benchi la ufundi litakapoiona litakuwa na chochote chakuzungumza,” alisema Kahemele.

Timu ya Simba itarusha kete ya kwanza katika ligi kuu ya msimu ujao kwa kucheza na Ndanda FC ya mkoani Mtwara, mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo pia utakuwa kipimo cha kwanza kwa Omog, raia wa Cameroon ambaye amerejea nchini kuinoa Simba iliyoweka kambi yake Morogoro na kujifua vikali, baada ya kuiongoza Azam FC kutwaa ubingwa wa ligi hiyo misimu miwili iliyopita.

Hata hivyo, wakati msimamo wa Simba ukiachwa kwa Omog ili kujua kama atapendezwa na ratiba hiyo au haitomvutia, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit amefafanua kwanini inawabana.

Katibu huyo ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), kusogeza mbele ratiba ya kuanza ligi kuu Tanzania Bara kwa kuwa imewanyima fursa wachezaji wao kupata nafasi ya kupumzika.

TFF, juzi ilitoa ratiba ya ligi kuu Tanzania Bara ambapo Yanga itaanza kwa kupambana na African Lyon Agosti 28, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ratiba hiyo pia inaonyesha Yaanga itacheza mchezo wa ufunguzi wa ngao ya Jamii Agosti 17, mwaka huu dhidi ya Azam FC.

Akizungumza jana, Deusdedit alisema ratiba hiyo imekuwa ngumu sana kwao kwa kuwa Yanga bado ina michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Timu hiyo iko kundi A na hivi sasa inajianda kwa ajili ya michezo ya hatua ya mzunguko wa pili.

Alisema kutokana na hali hiyo, timu yake inaweza ikashindwa kufanya vema kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na ligi hiyo kwa kuwa watakuwa hawajapata muda wa kupumzika.

“Ratiba tumeiona inaonekana kutubana sana japokuwa sisi tutachelewa kucheza na wenzetu wataanza Agosti 20 lakini bado haitupi nafasi ya kufanya maandalizi kwa ajili ya ligi,” alisema na kuongeza.

“Ukiangalia timu nyingine kwa sasa hazina michuano yoyote zimeanza maandalizi ya ligi lakini sisi bado tunapambana,” alifafanua Baraka.

Alisema TFF wanapaswa kujua kuna umuhimu wa wachezaji kupumzika kabla ya kuanza kwa ligi na kushauri ni vema wakasogeza mbele ratiba hiyo.

TFF YALONGA

Naye Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kuwa ratiba hiyo imezingatia michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa ngazi ya klabu na timu za taifa ili kukwepa dhana yoyote ya upangaji wa matokeo na kurundikana kwa michezo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.