Kichuya: Nataka kufunga, Mgosi mzuka umepanda

BURUDANI - - HABARI - NA NASRA KITANA

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Shiza Kichuya amesema ameipokea kwa mikono miwili ratiba ya ligi kuu msimu ujao na anachosubiri ni kufanya kazi iliyompeleka Msimbazi tu.

Akizungumza na gazeti hili kutoka kambini mkoani Morogoro ambako Simba imejichimbia kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao, Kichuya alisema hana tatizo na ratiba hiyo na anataka kuwapa raha wana Msimbazi na kocha Joseph Omog.

“Nimeiona ratiba mimi nataka kufanya kazi yangu uwanjani,” alisema Kichuya ambaye Simba imemsajili kutoka Mtibwa Sugar.

Wachezaji wengine wa Simba, Jamal Mnyate na Emmanuel Semwanza wote kutoka Mwadui FC wamesema kuwa wameiona ratiba na hawana hofu yoyote.

Walisema licha ya msimu unaokuja kuonekana kuwa mgumu kutokana na kila timu kujipanga vyema, lakini wametamba Simba wako fiti zaidi na wao wamepania kufanya mapinduzi ndani ya kikosi hicho.

“Tumekuja kufanya kazi na tutahakikisha tunapambana kadri tuwezavyo na kila timu tutakayokutana nayo ili tuibuke kidedea,” alisema Mnyate.

Wakati huo huo, nahodha wa timu hiyo Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema kuwa anaendelea kujipanga kupambana na wachezaji kutoka nje ya nchi kusaka namba katika kikosi cha kwanza.

Alisema kuwa anashukuru kwa uamuzi wa viongozi wa klabu ya Simba kuwapeleka mapema kambini.

Alisema anajifua kwa nguvu zote ili kuhakikisha msimu ujao anaonyesha kiwango chake.

“Unajua msimu uliopita, nilifunga bao moja, watu walisema sana, lakini watu hawaangalii nimecheza mechi ngapi, ngoja msimu ujao uanze, nionyeshe kazi,”alitamba Mgosi.

Hata hivyo, mchezaji huyo alisema kwa sasa ndani ya timu hiyo kuna changamoto nyingi kutokana na wachezaji wanaofanya majaribio kuwa katika kiwango kizuri.

“Hawa wananipa faraja na changamoto ya kujituma ili niweze kupamba nao, nina hakika msimu ujao nitafanya vizuri sana,”alisema Mgosi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.