Timu zijiandae kwa ligi kuu

BURUDANI - - MAONI / HABARI -

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza ratiba ya ligi kuu ya Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 20, mwaka huu.

Kabla ya kuchanwa pazia hilo, Agosti 17 Yanga na Azam FC zitacheza mechi ya Ngao ya Jamii ambayo ya ufunguzi wa ligi hiyo itakayoshirikisha jumla ya timu 16.

Tunasema ratiba hiyo imetangazwa wakati muafaka kwa timu zote ambapo sasa vizuri zifanye maandalizi ya kutosha kwa lengo la kufanya vyema msimu ujao.

Maandalizi hayo ni kila timu kufanya usajili bora, kuimarisha mabenchi ya ufundi, kukamilisha safu za uongozi na kutafuta mechi za kirafiki ambazo zitatoa mwanga wa uimara au udhaifu wao kabla ya kusubiri ligi ianze.

Upungufu utakapobainika mapema itawazindua viongozi kwa kushirikiana na mabenchi yao ya ufundi kufanya marekebisho ya kuondoa dosari hizo haraka na kuunda timu za kutoa ushindani kwenye ligi na sio kuwa wasindikizaji.

Ligi inapokuwa na timu wasindikizaji inakuwa hainogi kufuatia kukosekana ushindani unaotakiwa, ambao ukiwepo unakuwa daraja la kutoa wachezaji wenye viwango na kuunda timu nzuri ya taifa.

Tunaamini bila ya ligi imara timu ya taifa lolote haiwezi kuwa imara kwa sababu ya kuwa wachezaji wasio na maandalizi kabambe na kuepuka hilo, inapasa timu shiriki zijiandae ndio zitaweza kushindana kikamilifu na kufanya vizuri msimu ujao.

Maandalizi hayo yawe ya kuwaweka kambini wachezaji, kucheza mechi za kirafiki za ndani na nje ya nchi na kufanya tathmini vyao kabla ligi haijaanza kuliko kuingia kwenye michuano hiyo na timu legelege, ambayo itaishia kusindikiza na kushuka daraja.

Tunasema kila timu ikijiandaa vyema ligi kuu itakuwa bora kutokana na kushirikisha wachezaji wenye viwango staili na hata bingwa atapatikana kutokana na uwezo wa kucheza soka uwanjani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.