Bidvest kumwaga dola Jangwani

BURUDANI - - MBELE - NA NASRA KITANA

KLABU ya Bidvest ya Afrika Kusini, ipo mbioni kumuita kwa majaribio kiungo wa Yanga, Said Juma ‘Makapu’ ambapo kama atafuzu itamwaga mamilioni kwenye klabu hiyo.

Makapu anatarajia kwenda kufanya majaribio wakati wowote kuanzia leo baada ya mipango kwenda vizuri.

Akizungumza na Burudani, kiungo huyo, alisema muda wowote kuanzia sasa akirudi nchini Tanzania akitokea Ghana ambapo alikwenda na timu hiyo kucheza na Medeama, ataondoka.

Yanga ilikwenda Ghana kupambana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano.

Mchezo wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya kufunga bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Makapu alisema anaimani atatumia vizuri nafasi hiyo kwa kucheza kwa malengo zaidi ili aweze kutimiza ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa.

“Uwezo ninao na nia ninayo hivyo endapo nitafanikiwa kuondoka na kwenda katika timu hiyo kwa ajili ya majaribio sitaweza kuwaangusha Watanzania, kikubwa ni maombi yao ili niweze kufanya vizuri na kupata nafasi ya kucheza huko,” alisema.

Makapu alisema anaamini atafanikiwa na huo ndio utakuwa mwanzo wake mzuri wa kufikia mafanikio ya kucheza timu kubwa zaidi na kuisaidia Taifa Stars endapo ataitwa kuichezea.

Yanga ilimsajili Makapu mwaka 2014 akitokea katika timu ya Shangani FC ya Zanzibar, lakini alikuwa kivutio zaidi katika kikosi cha Taifa Stars Maboresho na kumpa mkataba wa miaka miwili. Mkataba huo umeisha mwaka huu na kuongezwa mwingine.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.