PLUIJIM AUWASHA MOTO YANGA

Bilioni 250 zamng’oa Higuain Napoli

BURUDANI - - MBELE - NA NASRA KITANA

BAADA ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana, kocha wa mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga, Hans van der Pluijm, amelaumu mabeki wake kwamba hawakufuata maelekezo aliyokuwa akiwapa.

Yanga walikuwa wageni wa Medeama katika mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika(CAF), ambao ulichezwa juzi katika Uwanja wa Sekondi, Tokoradi nje kidogo ya jiji la Accra, Ghana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kumalizika mchezo huo juzi, Pluijm alisema mabeki wake hawakufuata kile ambacho alikuwa anakieleza.

Alisema ubora wa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondan ambao aliwapanga katika mchezo huo, haukuonekana katika mchezo huo kwa vile hawakuwa mchezoni kabisa.

“Ukweli hawa mabeki wamecheza wanavyojua wao hawakufuata kabisa maelekezo ambayo nilikuwa nawapa, katika mchezo huu nimemkumbuka sana Vicent Bossou ambaye hakuwepo katika mchezo huu kwa sababu alikuwa na kadi mbili za njano hakika pengo lake limeonekana,” alisema.

Msafara wa mabingwa hao unatarajia kurejea nchini kwa mafungu ambapo wa kwanza ulitua jijini Dar es Salaam saa 7 usiku kuamkia leo, wakati msafara wa pili unatarajia kutua nchini saa 2 asubuhi.

Baada ya kurejea nchini, nyota wa Yanga watapewa mapumziko mpaka kocha atakapokihitaji kikosi kianze mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao.

Mabingwa hao watetezi, wanatarajia kuwa wenyeji wa mchezo ujao dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria, utakaochezwa Agosti 8, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga ilianza hatua ya robo fainali kwa kipigo cha 1-0 dhidi ya Mo Bejaia, ikapigwa 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikatoka sare na Medeama kabla ya kufungwa 3-1 katika mchezo wa marudiano.

Kwa vipigo hivyo, Yanga inakamata mkia katika msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi moja, Medeama ipo nafasi ya tatu kwa pointi tano huku TP Mazembe ikiongoza msimamo huo kwa pointi saba na Mo Bejaia ipo nafasi ya pili kwa pointi tano.

Msimamo huo ni kabla ya mchezo wa jana kati ya TP Mazembe na Mo Bejaia.

MJUMBE ANENA

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Hussein Nyika amesema kuwa kitendo cha timu hiyo kufungwa na Medeama kimetokana na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kutojituma ipasavyo na kusababisha kipigo hicho.

Alisema wachezaji wa Yanga, walishindwa kujituma ipasavyo na kusababisha kipigo hicho cha mabao 3-1 kutoka kwa timu hiyo ya Ghana.

“Nina hakika walifundishwa mbinu nyingi, lakini ilikuwa tofauti na mchezo waliocheza na Medeama, sijui labda kama binadamu huenda wachezaji wetu wamechoka kwani hawajapata muda wa kupumzika kabisa,”alisema mjumbe huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.