Ney wa Mitego afungiwa

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia msanii Emannuel Elbarik ‘Ney wa Mitego’ kutokujihusisha na sanaa kwa kipindi kisichojulikana pamoja na kumtoza faini ya sh. milioni 1 kufuatia kukiuka maadili ya kisanaa katika wimbo wake wa ‘Pale kati’. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa BASATA, Godfrey Mngerez a , alisema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kujadiliana kwa siku mbili na msanii Ney wa Mitego na kukubaliana kuwa adhabu hiyo itabadilishwa endapo atatekeleza baadhi ya masharti aliyopewa.

“Tumejadiliana tokea jana (juzi) na kufikia muafaka wa kumfungia msanii huyu kujihusisha na sanaa kwa kipindi kisichojulikana, pia tumemtaka kulipa faini ya fedha hizo na kurekebisha mashairi ya wimbo wake wa Pale Kati,” alisema Mngereza.

Baraza hilo, pia limemtaka Ney wa Mitego kuomba radhi kwa umma kutokana na maudhui ya wimbo wake kuonekana kudhalilisha utu hasa wa mwanamke na kumtaka ajirekebishe katika nyimbo anazotunga.

Msanii huyo, ametakiwa kurekebisha maudhui ya nyimbo hiyo ambao ulishafungiwa wiki mbili zilizopita.

Ney wa Mitego amekiri kufanya kosa hilo na kuomba radhi kupitia vyombo vya habari huku akikubali kutekeleza adhabu zote zilizoelekezwa juu yake ndani ya siku mbili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.