Makocha wageni watajwa TFF

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine ameziasa klabu za ligi kuu Tanzania Bara na daraja la kwanza, kutimiza masharti ya kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini wachezaji na makocha wa kigeni kabla ya kusaini nao mikataba ya ajira.

Amesema masharti hayo ni vibali vya kufanya kazi nchini, visa, vibali vya kucheza, kufundisha na vibali vya watalaamu wengine kama madaktari.

Mwesigwa alisema hayo ni matakwa ya Idara ya Uhamiaji na mamlaka nyingine za serikali na kanuni za TFF.

“Mchezaji au mtaalamu yeyote anapokuja nchini na kuanza mazoezi na timu yoyote anachukuliwa yuko kazini. Tusingependa watu wapate usumbufu. Kama Katibu Mkuu na mtendaji mkuu, nimepata maelekezo kutoka mamlaka zinazohusika kuwa nifuatilie kama mratibu mkuu wa mchezo wa mpira wa miguu TFF ina jukumu

la kuhakikisha wanachama wake wanafuata taratibu,” alisema.

“Klabu zihakikishe vyeti vya taaluma vinawasilishwa TFF kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kutiliana kandarasi na wachezaji au walimu. Ni vema wakafanya uratatibu

wa kuhakiki hii itaziepusha na gharama za fidia au kesi za madai endapo mamlaka za serikali au za mpira zitasita kumruhusu mhusika kufanya kazi nchini.”

Mwesigwa pia amezitaka klabu kufikia muafaka na wachezaji na wataalamu wanaoachana nao kabla ya kufikiria kuajiri wapya. Alisema TFF tayari ina barua kadhaa za madai ya wachezaji na watumishi wa klabu waliomaliza au kukatishwa mikataba bila kulipwa mafao yao.

Wakati huohuo, katibu huo ameagiza klabu kuendelea na usajili kabla ya Agosti 6, 2016 ambayo itakuwa siku ya mwisho na hakutaongezwa muda kwa klabu ambayo itashindwa kukamilisha usajili kwa wakati.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.