Masau Bwire achimbwa mkwara

BURUDANI - - HABARI -

UONGOZI wa timu ya Mtibwa Sugar, umemuonya Masau Bwire kuacha kufuatilia habari za timu nyingine na kueleza kuwa mdomo wake utaiponza Ruvu Shooting kushuka daraja.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru alisema jana kwamba ni vyema msemaji huyo wa Ruvu Shooting akaacha mambo ya kufuatilia habari za timu nyingine.

Alisema kitendo cha Bwire kufuatilia habari za timu nyingine kitasababisha kila timu kuipania Ruvu Shooting ili kuwapa dozi.

“Nimemsikia anasema juu ya Mtibwa, sisi hatuwezi na ninamshauri aangalie yasije yakamkuta kwa kushuka daraja tena, kama awali ilivyotokea, anawashtua wapinzani wake kujipanga ili kuisambaratisha timu yake,”alisema Kifaru.

Kauli hiyo, imekuja baada ya Masau Bwire kusema kuwa wamejipanga kuitungua Mtibwa katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu ujao ambapo timu hizo zitapambana.

Bwire alisema wanajua mbinu zote za Mtibwa kwa vile ina wachezaji wengi wadogo na wengine wamekuwa na umri mkubwa kitu ambacho wao watakitumia kuwakimbiza wapinzani wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.