MAVUGO awatangazia vita makipa

BURUDANI - - MBELE - NA NASRA KITANA

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba Leudit Mavugo amesema kuwa hajui idadi ya mabao atakayofunga, lakini ametamba yatakuwa mengi hivyo makipa wa timu zote 16 za ligi kuu wakae tayari kuokota mipira wavuni.

Alisema kuwa kufunga suala la kawaida kwake hivyo wana Simba wasubiri raha kwenye msimu wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mavugo alifunga bao moja kati ya manne yaliyofungwa na Simba dhidi ya AFC Leopards ya Kenya huku pia akishiriki katika upatikanaji wa mabao mengine mawili.

Simba ilipata ushindi huo mnono katika tamasha maalumu la ‘Simba Day’ ambalo lilifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam.

Akizungumza jana, Mavungo ambaye ni raia wa Burundi alisema kuwa huwa hana idadi ya mabao atakayofunga, lakini kufunga ndio kazi yake na kudai hawezi kumaliza mchezo bila ya kucheka na nyavu.

Alisema mechi dhidi ya FC Leopards ilikuwa nzuri kwa kuwa alipata ushirikiano kwa wachezaji wenzake kitendo ambacho kilimfurahisha na kuona yupo nyumbani.

“Muda umefika wa wanasimba kufurahi, na mimi pia nilikuwa nasubiria muda wa kutua Simba na ndio huu sina kingine cha kuwalipa mashabiki kwa sapoti walionionyesha bali nitacheza kadri ya uwezo wangu kuhakikisha nawapatia ushindi ndani ya timu yao,”alisema.

Simba imemsajili Mavugo akitokea Vital’O ambako amekuwa mfungaji bora wa ligi ya Burundi akifunga mabao 30 na ameonyesha ana hamu ya kutwaa kiatu cha dhahabu ambacho msimu uliopita kimebebwa na Mrundi mwenzake Amisi Tambwe.

Hata hivyo kumekuwa na uvumi wa kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Vital’O ya Burundi na kusisitiza jina la mchezaji huyo lipo kwenye orodha yao iliyokwenda CAF ndani ya shirikisho la soka chini Burundi kwa msimu ujao.

Inavyosemekana tayari klabu hiyo imeamua kuishitaki Simba FIFA kwa ajili ya kuingia mkataba na mchezaji ambaye bado yupo kwenye mkataba wa mwaka mmoja ambao unamzuia kufanya mazungumzo na klabu yoyote kuhusu usajili bila klabu husika.

Burudani lilimtafuta Mavugo na kuzungumzia madai hayo, lakini alisema hana mkataba wowote na klabu hiyo na hata alipokwenda kufanya majaribio Ufaransa alikuwa mchezaji huru.

“Mimi sina mkataba na timu yangu ya zamani nimeondoka nikiwa mchezji huru na ninavyoambiwa bado nina mkataba hilo linanishangaza sema rais wa klabu Bikolimana Benjamin alikuwa ananihitaji niendelee kwenye timu yake ila na mimi kwa sasa nahitaji kufanya mabadiliko kwani mpira ni kazi yangu na nipo hapa kwa ajili ya kutafuta hela,”alisema

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema kuwa si kweli mchezaji huyo walimchukua kwa kukiuka taratibu na yanayozungumzwa ni maneno ya mitaani kuwa Mavugo hajamaliza mkataba na klabu yake ya Burundi.

Wakati huo huo, kocha Joseph Omog atapata tena nafasi ya kukijaribu kikosi chake Jumapili katika uwanja wa Taifa watakapokuwa wenyeji wa URA ya Uganda.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.