Yanga yakwepa hujuma ya Waarabu

BURUDANI - - HABARI - NA WAANDISHI WETU

WAKATI mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga wakiwa wameingia kambini, wapinzani wao katika mchezo wa Jumamosi, MO Bejaia ya Algeria walitua nchini juzi na kujikuta wanapigwa chenga ya mwili na wapinzani wao

Yanga wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano hatua ya Nane Bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambao utachezwa Uwanja wa Taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alisema kikosi chao kiliingia kambini juzi katika hoteli ya Tiffany kujiandaa na pambano hilo, huku wakikwepa mbinu ya Mo Bejaia ambao walifika katika uwanja wa Boko Veterani ili kusoma mbinu zao na kushindwa kuambulia kitu.

Timu hiyo baada ya kujua Yanga iliwakwepa, walitumia uwanja huo kufanya mazoezi kujiweka fiti kusubiri mechi ya Jumamosi.

Yanga ambayo itacheza mchezo huo wa nne ikiwa na pointi moja, bado inaweza kushika nafasi ya pili nyuma ya TP Mazembe yenye alama 10 katika kundi la A. Mo Bajeia na Medeama zina pointi tano kila moja na Yanga pointi moja.

Yanga katika michuano hiyo wamepata matokeo mabaya ambapo walianza kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya MO Bejaia, wakafungwa tena 1-0 dhidi ya TP Mazembe na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama kabla ya kutandikwa 3-1 katika mchezo wa marudiano dhidi ya Medeama nchini Ghana.

Mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara, watahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji wao TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Agosti 23, mwaka huu.

YANGA WAJIFUA GYMKHANA

Akizungumzia walivyokwepa hujuma ya Bejaia, Baraka alisema kuwa Yanga imeingia kambini kujiandaa na mchezo huo na kufanya mazoezi ya nguvu katika viwanja vya Gymkhana.

Alisema wameweka ulinzi mkali ili kupanga mfumo wa kucheza siku hiyo na kuongeza kwamba viongozi na benchi la ufundi wapo makini kuhakikisha mchezo huo wanashinda ili waweze kufufua matumaini ya kusonga mbele.

“Najua kwamba hatujashinda hata mechi moja katika hatua hii, kwa sasa tunafanya kila liwezekanalo ili kushinda dhidi ya MO Bejaia, lakini kwa bahati mbaya kwenye mchezo huo tutamkosa Donald Ngoma ambaye anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano, lakini wapo wachezaji wengine watasaka ushindi,”alisema.

Yanga walikimbia Boko Veterani baada ya kusikia tetesi za kuwepo baadhi ya mashushushu wa timu hiyo ya Algeria unawasoma.

Wapinzani wao walipewa taarifa kuwa Yanga wanafanya mazoezi kwenye uwanja huo na kuvamia ambapo walishangaa kukuta ‘kweupee’ na kwenda kuweka kambi yao katika hoteli ya Ledger Plaza, Kunduchi iliyopo Dar es Salaam.

Timu hiyo ilitua nchini, juzi usiku ikiwa na msafara wa watu 30 wakiwemo wachezaji 21 na viongozi tisa, tayari kwa mchezo huo ambao utakuwa ni muhimu kwa Yanga.

Mbali na msafara huo, msafara mwingine wenye watu zaidi ya 50 wa mashabiki wa Mo Bejaia wanatarajiwa kutua nchini kesho kwa ajili ya kuwapa sapoti nyota hao kwenye mchezo huo.

Faraja kubwa ndani ya kambi ya Yanga ni kurejea dimbani beki wao kisiki Kelvin Yondani aliyekuwa majeruhi pamoja na Vicent Bousou ambaye alikosa mchezo wa mwisho dhidi ya Medeama kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

WAAMUZI/VIINGILIO VYATAJWA

Mchezo huo, umepangwa kuchezeshwa na waamuzi kutoka nchini Ethiopia ambapo katikati atakuwa Bamlak Tessema Weyesa akisaidiwa na Kindie Mussie na Temesgin Samuel Atango wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Haileyesus Bezezew Belete.

Kamishna atakuwa Gaspard Kayijuka kutoka nchini Rwanda wakati Desire Gahuka wa Burundi atasimamia ufanisi wa waamuzi na Mratibu Mkuu ni Isam Shaaban kutoka Sudan.

Mratibu huyo alitarajiwa kuwasili nchini jana wakati waamuzi watatua leo huku msimamizi wa waamuzi atatua kesho.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema viti vya rangi ya kijani, bluu na chungwa viingilio vitakuwa sh 3,000, wakati VIP A kiingilio kitakuwa sh. 15,000 huku B na C ikiwa sh. 10,000.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.