Manji apeta Yanga

BURUDANI - - MBELE - NA SOPHIA ASHERY

WAKATI Baraza la Wadhamini la klabu ya Yanga likitarajiwa kukutana kesho, imedokezwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, anapeta kwa asilimia 90 ya kukubaliwa ombi lake la kuikodisha timu hiyo pamoja na nembo.

Baraza hilo ambalo linaundwa na wajumbe Mama Fatma Karume, George Mkuchika, Balozi Ami Mpungwe, Jabir Katundu na Francis Kifukwe, litakutana kesho kujadili barua ya Manji ya kuomba kukodisha timu hiyo na nembo ya klabu ya Yanga kwa kipindi cha miaka 10.

Kwa mujibu wa habari kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, ‘vigogo’ hao watakutana na kujadili barua aliyoiandika Manji kuomba ridhaa ya wadhamini kuikodi timu hiyo.

Mjumbe huyo alisema baraza litakutana baada ya Mama Karume kurejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini kwa mapumziko.

Alisema baada ya kukutana, wajumbe wa baraza hilo watajadili barua ya Manji kabla ya kutoa uamuzi ambao utapelekwa kwa wanachama kwa maamuzi zaidi.

“Tunakutana kesho ili kujadili barua ya Manji lakini katika mazungumzo ya awali ambayo yaliyofayika wiki moja iliyopita asimilia 90 wajumbe walionyesha kukubali wazo la kuikodisha timu kwa mwenyekiti ila baraza litatoa hitimisho kesho baada ya kujadili kwa kina hivyo ni bora kuvuta subira,” alisema mjumbe huyo.

Hata hivyo, alisema licha ya kujadili barua hiyo, baraza la wadhamini halitauharakisha mchakato huo na itaufanya hatua kwa hatua ili wadau wote wa klabu hiyo wawe na uamuzi ambao hautakuwa na lawama kwa upande wowote.

Alipoulizwa kuhusu kikao hicho, Katibu wa Yanga Baraka Deusdedit, alisema yupo kwenye kikao hivyo atafutwe baadaye na alipopigiwa tena hakupokea simu.

Wakati baraza la wadhamini likikutana kesho, uongozi wa klabu hiyo umewaita wadau na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kushirikiana kibiashara.

Mkutano huo wa wadau utafanyika katika hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, Dar es Salaam na kusema lengo la mkutano huo ni kujadili na kuwaelewesha jinsi ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya klabu hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.