Mbwana Samatta awateka Nigeria

BURUDANI - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea timu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amekuwa gumzo nchini Nigeria ambapo baadhi ya mashabiki wanataka kumfahamu baada ya kuwa tishio kwenye ligi kuu ya Ubelgiji.

Mchezaji huyo kabla ya kutua Genk, aliwahi kuwa mfungaji bora wa michuano ya klabu bingwa Afrika msimu uliopita, amekuwa gumzo nchini Nigeria ambapo mashabiki wanataka kumuona baada ya kuonyesha uwezo mkubwa.

Akizungumza jana kutoka nchini Nigeria, Mwenyekiti wa Chama Wachezaji Soka Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kisoki ambaye ametangulia nchini humo kwa ajili ya kuweka sawa mazingira kabla Taifa Stars kuwasili, alisema watu wamekuwa wakimzungumzia mchezaji huyo.

Kisoki jana usiku alitarajiwa kumpokea mchezaji huyo ambaye alitoka nchini Ubelgiji kupitia London, Uingereza kwa ajili ya kuwasubiri wachezaji wenzake ambao wanaotarajiwa kuondoka nchini leo alfajiri na kufika Nigeria usiku.

Alisema baadhi ya wapenzi wa soka nchini Nigeria, wamekuwa wanamuulizia Samatta kutokana na kuwa tishio hivi sasa kufuatia kufanya vyema Ubelgiji na michuano ya kufuzu Europa Ligi.

Samatta aliwahi kucheza katika timu ya Mbagala Market, Africa Lyon, Simba na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Taifa Stars, imeenda kupambana na Nigeria Jumamosi hii katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2017, zitakazofanyika nchini Gabon, mwakani. Katika kundi hilo Misri imeshafuzu.

Wakati hayo yakiendelea nchini Nigeria, jijini Dar es Salaam jana, beki Kelvin Yondani wa Yanga ndiye pekee ambaye hakuripoti kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichopiga kambi kwenye Hoteli ya Urban Rose.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema wachezaji wote wa timu hiyo waliripoti kambini isipokuwa mchezaji huyo, huku kipa Said Kipao akijiunga na timu hiyo mara moja baada ya kuteuliwa na kocha mkuu, Charles Mkwasa.

Kikosi Stars ambacho kimeondoka leo alfajiri ni makipa, Said Kipao (JKT Ruvu) na Aishi Manula (Azam FC), mabeki ni Andrew Vicent ‘Dante’ na Mwinyi Haji wote wa Yanga, David Mwantika na Shomary Kapombe (Azam) na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba).

Viungo, Himid Mao (Azam), Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya na Jamal Mnyate wote wa Simba, Juma Mahadhi na Simon Msuva (Yanga) pamoja na Mohammed Ibrahim ‘Jeba’ (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni John Bocco na Farid Mussa (Azam) na Ibrahim Ajib (Simba).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.