Hassan Kessy, Simba ngumi mkononi

BURUDANI - - MBELE - NA NASRA KITANA

FILAMU ya beki wa Yanga, Hassan Kessy na Simba imefika pabaya baada ya kile kinachodaiwa viongozi wawili wa klabu hiyo kutaka kurusha ngumi kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa sakata hilo kikaoni.

Uongozi wa Simba umeapa kuhakikisha unapigana kufa au kupona ili kupata haki yao ambayo inadaiwa wanahisi inataka kupotea kutokana na uamuzi ambao unaelekea kutolewa.

Chanzo cha uhakika kimesema kwa sababu hiyo Simba imepanga kubeba faili lao kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF) ili kulipeleka shirikisho la soka duniani (FIFA) endapo haitaridhika na uamuzi utakaotolewa Jumapili na Kamati ya Hadhi na Maadili ya Wachezaji.

Tayari Simba imewasilisha vielelezo vya Kessy juu ya tuhuma za kuvunja mkataba kwa kujiunga na Yanga kabla ya mkataba wake kumalizika jambo ambalo wanasisitiza alikiuka sheria.

Uongozi wa Simba ulipeleka vielelezo hivyo kwenye kikao kilichofanyika Agosti 29, mwaka huu, kilichofanyika kwenye ofisi za TFF, zilizopo Karume, Ilala, Dar es Salaam na shauri hilo lilianza kusikilizwa kuanzia saa 3:00 asubuhi na kumalizika saa 9 adhuhuri na kukosekana muafaka kufuatia pande hizo mbili kutaka kupigana mara tatu.

Kikao hicho cha kamati kiliongozwa na mwenyekiti Wilson Ogunde wakati Simba waliwakilishwa na Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope.

Kessy aliwakilishwa na meneja wake, Athumani Tippo na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Soka nchini (SPUTANZA), Mussa Kisoki.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya kikao hicho, upande wa Kessy umeshindwa kutoa uthibitisho wa tuhuma dhidi yao ya kuvunja mkataba, lakini Simba walipeleka magazeti yote ambayo yalionyesha Kessy alijiunga na Yanga kabla ya kumalizika mkataba wake Juni 15, Mwaka huu.

Beki huyo alisaini mkataba huo, Mei 9, mwaka huu na Yanga lakini aliibukia katika fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Azam FC iliyopigwa Mei 25, mwaka huu katika dimba la Taifa, Dar es Salaam na kuvalishwa jezi kama ishara kuwa tayari ni mchezaji halali wa Yanga wakati mkataba wake na Simba ulikuwa bado haujamalizika hadi ilipofika Juni 15, mwaka huu.

Pia Kessy alijiunga katika msafara wa Yanga kwenda kuweka kambi nchini Uturuki ikiwa ni maandalizi kujiandaa na mechi dhidi ya MO Bejaia ya Algeria katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, msafara huo uliondoka nchini Juni 13, mwaka huu ikiwa ni siku mbili kabla ya mkataba wake kumalizika.

Tippo alisema kuwa beki huyo, aliingia mkataba wa kucheza Yanga, Juni 20, mwaka huu wakati kipindi hicho, tayari amemaliza mkataba na Simba licha ya picha zake kusambaa katika mitandao kumuonyesha akiwa na Yanga kabla ya siku hiyo.

Wakati huo huo Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara alisema jana kwamba wapo mbioni kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Hassan Kessy kwa kile alichoeleza kuwa amewatuhumu baadhi ya viongozi wa timu hiyo ya Msimbazi walitaka kumpa rushwa mchezaji huyo wakati anaichezea Mtibwa Sugar.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuona mchezaji huyo anatoa uthibitisho kuwa nani alitaka kumpa hongo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kessy alijiunga na Simba Desemba 2014 kwa mkataba wa miezi 18, akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.