Miaka 50 ya soka letu, je tumepiga hatua?

BURUDANI - - MBELE - NIACHE NISEME Na Haji S. MANARA

MWAKA 1966 ndio mwaka tulioanza kuwa na michuano ya kumtafuta bingwa wa mchezo wa soka nchini.

Pia ndio mwaka ambao ushabiki wa mchezo huu ulipoanza kushamiri kisawasawa hususani kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga.

Achana na hayo, huo ndio mwaka ambao Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilipoanza kuwa na makucha rasmi ya kusimamia mchezo huu unaopendwa na kuthaminiwa kuliko wowote nchini na duniani kwa ujumla.

Bila shaka lazima tujitathmini kama taifa, je tumerudi nyuma au tumesonga mbele? Au tupo pale pale?

Na hii nazungumzia soka kwa ujumla siyo ligi pekee ambayo klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam ndiyo iliyoanza kubeba taji la ubingwa wakati huo ikiitwa ligi ya taifa na ikichezwa katika vituo na kisha kuingia kwenye mtoano hadi bingwa kupatikana.

Zama hizo hatukuwa na miundombinu ya viwanja kama tuliyo nayo leo hii.

Hatukuwa na makocha wala waamuzi wanaozijua sheria za soka kwa wingi na wala hatukuwa na viongozi wasomi wanaoongoza mchezo huu.

Klabu zetu pia hazikuwa na vifaa bora vya wachezaji kuvitumia na sio kwenye mechi, bali hata mazoezini.

Hatukuwa na wadhamini wala wafadhili wa kuendesha mchezo huu murua kabisa duniani.

Pia hatukuwa na utitiri wa vyombo vya habari vya kuripoti soka wala hatukuwa na ‘blogs’ na wachambuzi wanaouchambua mchezo wa soka ambao inaaminika umevumbuliwa nchini China na kutungiwa sheria katika nchi ya Uingereza mwishoni mwa karne ya 18.

Kifupi kwenye maeneo hayo tumepiga hatua kubwa mno isiyo na mfano na ukweli lazima tujipongoze sana kwa hapa tulipofikia.

Tujiulize, je hatua hizi tulizopiga zinaenda pamoja na kukua mchezo wenyewe wa soka nchini?

Je, miaka 50 hii tunalo la kujivunia kimataifa kama nchi? au je, ligi yetu imekuwa bora kwa viwango vinavyostahili?

Je klabu zetu zina uwezo thabiti wa kushindana na timu za mataifa mengine hususani barani kwetu Afrika?

Je zinaweza kuwa nyingi kiasi cha kujaza makala nzima unayoisoma msomaji wangu mpendwa.

Kiufupi ‘JE’ hizi zina majawabu ya HAPANA tu. Vyovyote msomaji ukijaribu kudadavua utakuwa na jibu la hapana ambalo litakidhi majibu ya swali langu.JE?

Bahati nzuri mchezo wa mpira wa miguu huchezwa hadharani na matokeo yake tunayoona na kuyasikia watu wote.

Na bahati mbaya kwetu kama nchi, tuna machache mno ya kujivunia kwenye soka ukilinganisha ukubwa wa taifa letu na umri tulionao hususan huu wa miaka 50.

Fanikio la maana kabisa ambalo tumelipata, ni kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 zamani zikiitwa mashindano ya mataifa huru ya Afrika.

Sana sana kuchukua ubingwa wa kombe la Chalenji mara tatu, kombe ambalo hushirikisha nchi zilizopo Afrika Mashariki na Kati.

Sambamba na klabu zetu za Simba, Yanga na Azam kuchukua ubingwa wa kombe la Kagame ambalo nalo hushirikisha klabu za ukanda huu ulio nyuma zaidi kisoka ndani ya bara letu hili la Afrika.

Ukiacha mafanikio hayo madogo, Simba ilishawahi kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na pia nusu fainali ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974 sanjari na kucheza hatua ya makundi ya mabingwa wa Afrika 2003, ambayo pia Yanga walicheza hatua hiyo 1998, mbali ya mwaka huu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Siyajui mafanikio mengine rasmi tuliyoyapata kama taifa, zaid ya Simba kuzifunga timu kubwa za mataifa yaliyoendelea kisoka barani Afrika, kama yapo ni yale yasiyoingia kwenye kumbukumbu rasmi za mafanikio.

Bahati mbaya kwangu sina rika la kuona kilichotokea miaka 60 au 70 ila historia ipo na huo ndio ukweli usiopingika.

Ukinibana sana msomaji utaniambia Simba na Yanga zilishawahi kucheza na klabu kubwa za Brazil na Uingereza kisha kuzisumbua kwenye uwanja wetu wa Uhuru siku, zamani taifa.

Najua miaka ya 70 klabu kubwa kama West Bromwich Albion, Aston Villa, Norwich City na Cardiff City za Uingereza zilikuja hapa nchini na kuonyeshwa jinsi tulivyokuwa mahiri katika kucheza soka.

Ikumbukwe Aston villa ilikuja ikiwa bingwa wa kombe la FA la nchini kwao na ikabanwa kwa sare ya bao 1-1 na mabingwa wa sasa nchini Yanga.

Huku West Bromwich ikija na Waria Geoff Hurst aliyekuwa mhimili wa ushindi wa kombe la dunia ambalo Uingereza ililitwaa mwaka 1966.

Mbali ya klabu hizo za Uingereza, klabu kadhaa za nchini Brazil zilikuja miaka hiyo ya 70.

Mojawapo ya klabu hizo ni Fluminense, ABC na Colarado ilioifunga Yanga 4-0 huku siku hiyo ikimtumia kipa bora wa muda wote nchini Athuman Mambosasa aliyejiunga kutokea Simba, klabu aliyoitumikia kwa muda mrefu.

Pia timu ya taifa ya vijana ya taifa ya Brazil ikiwa na nyota wa fainali za kombe la dunia la mwaka 1982 Serginho, ilikuja nchini na kucheza michezo kadhaa za kirafiki.

Nikukumbushe pia ujio wa FC Lugano ya Uswisi na klabu za kutoka nchini Romania zilifanya ziara hapa nchini na kuonyeshwa cha moto na Simba na Yanga.

Watakaonipinga watasema hayo nayo ni mafanikio makubwa na mimi nisiwapinge, ila tukubaliane hayakuwa mafanikio rasmi ukizingatia mechi zote walizocheza zilikuwa za kirafiki.

Nilishawahi kujiuliza mara kadhaa kwa nini miaka ile ya 1970 hatukuwa tunafuzu kwenye Afcon au kombe la dunia?

Huku tukiwa tunao uwezo wa kuzifunga timu kubwa za Ulaya na Brazil.

Hili swali licha ya kujiuliza na kuwauliza watu kadhaa, nimeshindwa kupata jibu la moja kwa moja ila kwa utafiti wangu, nimegundua hakukuwa na hamasa kwenye timu ya taifa kwa upande wa viongozi wa FAT na serikali.

Klabu zenyewe pia zilijikita zaidi kwenye upinzani wao wa jadi, hususan wa Simba na Yanga.

Nilishawahi kuambiwa kuna wachezaji walikuwa wanakataa kuchezea timu ya taifa hususani wa hizi klabu kubwa na majibu yao ya kukataa ni kuwa Simba na Yanga ni kubwa kupita timu ya taifa!

Kiukweli nchi hii imeshawahi kushuhudia vipawa vya ajabu vya wachezaji, sijui msomaji kama ushabahatika kumsikia Mbwana Abushiri’Director’, Emily Kondo, Peter Tino au Omari Zimbwe?. Watu hawa tunaambiwa uwezo wao haukuwa na mfano.

Tukirudi katika mada bado mafanikio tuliyopata hayalingani na kiuhalisia na miaka 50 ya uwepo wa mchezo huu rasmi toka tumeingia kwenye ligi.

Najua umeshawahi kusikia kuhusu Maulid Dilunga, Abdallah Kibadeni, Gibson Sembuli na Kitwana Manara na nduguze Sunday na Kassim Manara.

Hao ni wachezaji wa miaka ya 1960 hadi 1970 tena niliowataja ni wachache tu miongoni mwa wachezaji bora kabisa kutokea nchini.

Hapo sijakutajia wa kizazi cha dhahabu cha Lagos 1980, Mambosasa, Leodegar Tenga, Jellah Mtagwa, Mohammed Rishard, Salim Amir, Hussein Ngulungu, Mohammed Salim, Peter Tino na wengineo.

Pia sijakukumbusha mwamba wa nyavu nchini Zamoyoni Mogela au kiungo bora wa miaka ya 1980 na 1990 marehemu Hamis Thobias Gagarino.

Wala sijakutajia kile kizazi cha miaka ya 1990 kikiongozwa na Mohammed Mwameja, Hussein Marsha, George Masatu, Athuman China, Edward Chumila, Ally Maumba na wengine.

Kiukweli tulikuwa na vipaji ambavyo vingeweza kucheza kokote duniani.

Lakini sijui kwa nini ilishindikana na sijui kwa nini havikuunganishwa kutupa matokeo tuliyokuwa tunastahili kwenye klabu zetu na timu ya taifa?

Jibu lake mimi na wewe hatulijui na hatuna cha maana tulichofanya.

Inasikitisha na inaumiza nchi kama hii haijawahi kuchukua ubingwa wa klabu Afrika.

Hatujawahi kufuzu kombe la dunia ilhali nchi ndogo kama Togo na Senegal zilishawahi kufuzu, lakini linalokera zaidi hatuna mkakati kama taifa kupata mafanikio hayo.

Hivi mnajua nchi hii haijawahi kufuzu hata fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 au 21?

Achana na kufuzu Michezo ya Olimpiki ambayo hushirikisha vjana walio na umri chini ya miaka 23.

Ni fedheha kama taifa kushindwa kupata kile ambacho tunastahili kama tungekuwa tuna mipango madhubuti.

Nikuombe msomaji wangu jiandae kusoma makala zangu zijazo juu ya changamoto hizi na maoni ya kuondoka hapo tulipo na kwenda mbele zaidi.

Leo nilielezea historia fupi ya huko tutokapo lakini wiki ijayo makala hii itaendelea na kuzungumzia nini tufanye ili na sisi siku moja tufike kwenye mafanikio.

Mwisho niwaahidi kuwa makala zangu zitakuwa zinajadili hoja zaidi na siyo ushabiki na hazitaingiliana na majukumu ya kazi kwenye klabu yangu niipendayo na ninayoitumikia ya Simba. Tukutane wiki ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.