Msuva: Nina kazi kwa Yanga hii

BURUDANI - - HABARI -

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Simon Msuva, amesema kwamba ana kazi kubwa ya kuhakikisha anapata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, kufuatia kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.

Mchezaji huyo alieleza hayo wakati akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwa kutokana na hali hiyo, inabidi afanye kazi ya ziada kuhakikisha kiwango chake kipande zaidi.

Alisema kitendo cha kuwepo wachezaji wengi wazuri ndani ya Yanga, kinazidi kumpa kazi ya kujifua zaidi ili aweze kumshawishi kocha wa timu hiyo Hans Van Der Pluijm kuonyesha kiwango kikubwa ili aweze kumpa nafasi ya kucheza.

“Unajua Yanga kuna wachezaji wengi wazuri, akianza fulani na akitoka basi yule anayeingia anaweza kubadilisha matokeo ya mchezo na kusababisha timu kuonyesha soka safi na kupatikana ushindi, hapo inabidi kila mchezaji kuongeza bidii,”alisema.

Kauli hiyo, imekuja baada ya kocha wa timu hiyo kuonyesha kufurahishwa na uwezo wa kinda Juma Mahadhi ambaye katika mchezo dhidi ya African Lyon alimweka benchi ili kusoma mbinu za wapinzani wao kabla ya kumuingiza uwanjani kuchukua nafasi ya Msuva na kufunga bao la tatu ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 3-0.

Lakini ushindani mkali umekwepo kati ya nyota hao, huku ukiwahusisha Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Matheo Simon , Amissi Tambwe, Deus Kaseke na kinda Yussuf Mhilu, jambo ambalo limempa hofu Msuva.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.