Wanasubiri panga la Mourinho

Panga la Mourinho

BURUDANI - - MBELE -

KLABU ya Manchester United itahitajika kuwaondoa baadhi ya nyota wake katika dirisha dogo la usajili Januari.

Japokuwa mchakato wa usajili sasa umefungwa na kupunguza tetesi za nani anakwenda wapi na yupi anaingia, lakini Manchester United kwao hakukaliki.

Moto unawaka na mpaka uzimike lazima baadhi ya mastaa wapigwe panga kupitia mkono wa kocha Jose Mourinho.

Mreno huyo anataka kuleta damu changa klabuni hapo katika usajili wa Januari.

Kama atatimiza lengo hilo, kuna wachezaji hawataweza kupona ili kutoa nafasi kuletwa sura ngeni.

Si majina mengi kwa Mourinho ambayo wenyewe wanafahamu kuwa Mreno huyo maarufu kwa jina la Special One, atawatimua klabuni kwake.

Katika listi ya wachezaji wanaotarajia kupewa mkono wa kwaheri Januari, jina la Bastian Schweinsteiger halimo kwa sababu kwake kuondolewa klabuni hapo si suala la mjadala bali ni suala la muda tu. Ukifika ataambiwa, “Ahsante kwa huduma, karibu tena”

Utashangaa kati ya majina matano ya wachezaji wanaotakiwa kusepa Manchester United wengine ukiwajua hautaacha kushtuka na kuhoji kwa nini. Ndio hivyo kwao Januari imekaa vibaya!

MEMPHIS DEPAY

Winga huyu chipukizi amecheza mara moja tu chini ya kocha Mourinho, aliingia kutokea benchi kwa mantiki hiyo ana uhakika wa kuuzwa Januari.

Hawezi kuondoka bila ya kupokea ofa nono, lakini kuna klabu ‘saizi yake’ ambazo inaaminika zinatosha kwa Memphis kuonyesha kipaji alichonacho.

Ukweli, Memphis si aina ya mchezaji anayemvutia Mourinho. Kwanza, ni kinda, hajaonyesha ubora wake kuwa anaweza kufanya vitu kwa kocha huyo anayekunwa mno na wachezaji wakongwe.

Pili, ni mshambuliaji anayetia wasiwasi kuhusu kiwango chake cha kuzuia. Kutoweza kukaba ni suala lisilomvutia kocha huyo.

Ndio maana wachambuzi wengi, wanafikiri Memphis ataondoka majira haya ya kiangazi. Badala yake, Mourinho akiamua kumbakisha hiyo itatokana na kuwanyamazisha wanaomlaumu kwa madai hatoleta chipukizi yeyote katika klabu hiyo.

DALEY BLIND

Hana tofauti na Memphis, Daley Blind amepata nafasi kidogo sana ya kucheza kwa Mourinho. Kwanini, pengine ameandaliwa safari January?

Ataondoka kwa kuwa tu katika nafasi yake atakiwa beki nguli haswa atakayefaa kwa Man United.

Mashetani Wekundu wanahusishwa na wazo la kurusha ndoano kwa Raphael Varane na Fabinho hata baada ya dirisha la usajili kufungwa. Kama Mourinho ana dhamira ya kuleta mchezaji kama Varane, ina maana Blind ataondoka zake tu.

Asipoondoka Blind ataweza kutumika kama chaguo la pili, lakini haionyeshi kama atakuwa na uwezo japo kumshawishi Mourinho ili abaki. Ameonyesha kuwa anafaa kucheza ligi kuu England katika kikosi cha kwanza cha timu yoyote ila sio Manchester United. Ajaribu kwingine Ulaya.

ANDER HERRERA

Ni wakati wa kukabiliana na ukweli. Ander Herrera ni mchezaji wa wastani wa kucheza ligi kuu ya England. Ameonyesha kipaji, lakini kukosa ukomavu wa kucheza katika klabu ya kiwango cha Man United.

Kuna ubishani kuwa anastahili kubaki uimara wake, lakini United inaweza kununua kila mchezaji wa aina yake na kuozea benchi. Hatakiwi kubaki Old Trafford.

Herrera si mahiri vya kutosha kulinganisha na viungo wenye vipaji mfano wa Paul Pogba na Anthony Martial. Kwa sababu hiyo atafute klabu ya kiwango chake Januari.

MORGAN SCHNEIDERLIN

Huyu ana uhakika wa kufurushwa United. Ni kiungo raia wa Ufaransa ambaye hajaonyesha ubora wowote Old Trafford, ila kwa kiwango chake sio wa kudharauliwa moja kwa moja.

Schneiderlin alistahili kucheza na Pogba katika kikosi cha Mourinho. Chakusikitisha, kocha huyo ameamua kumtumia Marouane Fellaini badala yake.

Tottenham walijaribu kumwania siku ya mwisho ya usajili, lakini Mourinho alimbakisha kwa ajili ya michuano ya Europa Ligi. Pamoja na hayo uwezo wake sio wa kuaminika kuwa atakuwa juu msimu wote.

Mfaransa huyo kama asipotwaa namba kwa Fellaini mpaka January, mambo kwake yatabadilika. Schneiderlin atashinikiza kuuzwa ili apate nafasi ya kucheza mara nyingi, na Man United wanaonyesha kama watanunua mchezaji wa hadhi ya dunia mwenye uwezo sawa na Pogba.

JUAN MATA

Wakati kocha Mourinho alipotangazwa ni bosi wa Man United, wengi walitarajia Mata angeondoka mara moja klabuni hapo. Kisa mgogoro wake na kocha huyo, ambao ulikuwa mkubwa.

Amini kwamba Mourinho yupo sahihi kuhusu Mata kuwa ni mchezaji mpenda starehe, ndio maana sio rahisi wawili hao kufanya kazi pamoja. Klabu ya Man United itakuwa radhi kumkingia kifua kocha wao mpya kuhusu kumwambia kiungo huyo kwaheri ya kuonana.

Chakushangaza, Mhispania huyo ameanza mechi zote tatu cha ligi kuu England msimu huu. Hilo linaweza kuwashawishi baadhi kuwa Mata hatoki kwenye klabu hiyo, lakini kuwaza hivyo ni ujinga.

Mata anakosa sifa ya uanamichezo na kiwango chake cha kucheza cha kawaida na muda si mrefu atarushiwa lawama na wanazi wa Man United kwa sababu ya kiwango kuwa kidogo.

Bahati mbaya kwa Mata, kiwango chake cha kucheza kinapanda na kitamfaidisha kuuzwa kwa bei kubwa kwenye dirisha dogo au majira ya baridi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.