Kilimanjaro Queens yachimbwa mkwara

BURUDANI - - HABARI - NA DEUSDEDIT UNDOLE

KOCHA wa timu ya taifa ya soka ya wanawake Zanzibar, Nasra Juma amesema hawaihofii timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens kama watakutana nayo kwenye michuano ya Chalenji.

Michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza na kuzishirikisha nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (CECAFA), imepangwa kuanza Septemba 11, mwaka huu mjini Jinja, Uganda.

Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka kisiwani Zanzibar, kocha Nasra alisema hawana hofu na timu hiyo japokuwa alikiri Kilimanjaro inaundwa na wachezaji bora.

“Hakuna ubishi kwamba Kilimanjaro wana uzoefu mkubwa na michuano mbalimbali ya kimataifa ikilinganishwa na timu ya Zanzibar. Lakini kamwe sababu hiyo haitufanyi kuihofia,” alisema Nasra.

Alisema amewafundisha wachezaji wengi wa Kilimanjaro katika timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, ila anaamini wachezaji wake wamefanya maandalizi mazuri tayari kukabiliana na timu yoyote.

Kocha huyo alisema michuano hiyo ya CECAFA itawasaidia wachezaji wake, hasa wanaounda timu ya Zanzibar, kupata uzoefu wa michuano ya kimataifa.

Nasra alisema hata kama timu yake ikifanya vibaya, itakuwa imejifunza mengi kutoka kwa timu bora ambazo itakutana nazo kwenye michuano hiyo ikiwemo Kilimanjaro Queens.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.