Unyama unyama

BURUDANI - - HABARI - NA WAANDISHI WETU

PRESHA ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini timu za Simba na Yanga, imepanda zaidi kwa makocha wa klabu hizo, wachezaji, mashabiki na viongozi.

Kuonyesha kwamba presha inakaribia kufika 280 ambayo sio ya kawaida kwa mwanadamu yeyote, matajiri wa klabu hizo wamekimbilia benki kuchota fedha kisha kuweka mezani kwa ajili ya kuwapandisha molari wachezaji ili washinde Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Labda kwa kukumbusha tu Jumamosi ni keshokutwa siku ambayo itakuwa ya hukumu kwa Simba au Yanga zenye rekodi mbalimbali katika soka hapa nchini.

Kuonyesha kwamba mchezo utakuwa mgumu na kila upande ukipania kushinda, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba , Zacharia Hanspope ameahidi kutoa zawadi ya gari lenye thamani ya sh milioni 16 kwa kila mchezaji atakayefunga bao Jumamosi.

“Kila atakayefunga ni lazima apate gari yake mpya maana mwaka huu hatutaki masihara na tumejipanga na wachezaji wetu lazima wajivunie jasho lao,” alisema Hanspope.

Pia alisema Simba ikishinda pambano hilo wachezaji wote kila mmoja ataondoka na sh milioni 1.5 za kufurahia ushindi huo dhidi ya Yanga.

Ahadi hizo ni sehemu ya mwendelezo wa kile kilichofanywa na mjumbe huyo wa Simba ambaye mwezi huu alimzawadia gari aina ya Raum beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, sasa zawadi hiyo inaangukia kwa ambaye atafunga bao jingine.

Wakati matarajio ya wengi kuwa magari hayo yataangukia kwa washambuliaji mwiba Laudit Mavugo, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib, si ajabu Tshabalala akaondoka na gari la pili kutoka mikononi mwa Hanspope endapo na yeye atakuwa miongoni mwa wafungaji katika mechi dhidi ya Yanga.

Zawadi hiyo imeongeza ari kwa wachezaji wa Simba, ambao msimu huu kwao habari ni njema sana baada ya baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu ya tano chini Rais Dk. John Magufuli na wabunge kadhaa, kuchanga kitita cha sh milioni 50 na kuweka mezani kwa ajili ya nyota wao.

Tayari makundi hayo yamechanga fedha hizo na kuziweka ili timu hiyo ya Msimbazi itakaposhinda wachezaji wapate mgao wao.

Uchangiaji wa fedha hizo ulianza tangu ligi ianze ambapo kila mechi wachezaji wamekuwa wakipewa sh. milioni 10 kama motisha.

Simba wamepiga kambi mkoani Morogoro katika Chuo cha Biblia kujiandaa na mchezo huo ambao kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, watu wengine hawapendi hata kuusikia kwa hofu ya timu yao kufungwa, japokuwa soka ina matokeo matatu; kushinda, kufungwa au sare.

Asilimia kubwa ya mashabiki wa Simba na viongozi wao wanacheeka kwa kuamini Yanga hatoki katika mechi hiyo hasa baada ya washambuliaji wao kutupia na kuwemo kwenye safu ya washambuliaji. Mpaka sasa Kichuya anaongoza kwa kufunga mabao manne anafuatiwa na Mavugo mwenye matatu.

Pia Simba inaongoza ligi kwa kufikisha pointi 16 na mchezo wake wa mwisho kabla ya kutimkia kambini iliifunga Majimaji mabao 4-0.

YANGA SC KUNANI

Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, walikwea ‘ pipa’ hadi Pemba ambako wameweka kambi maalumu kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba.

Katika kambi yao wameweka ulinzi mkali ili kuhakikisha mtu asiyehusika haiingii eneo lao.

Kuonyesha kwamba mchezo huo unawapasua kichwa na hawataki kupigwa dozi nyingine kama iliyowakuta kwa wapiga debe wa Shinyanga, kocha Hans van Pluijm jana baada ya kumaliza mazoezi ya nguvu, alikaa na wachezaji wake zaidi dakika 360 ili kufanya uchambuzi wa mechi iliyopita na kurekebisha upungufu uliojitokeza.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, amekuwa mkali kwa wachezaji wote na katika uchambuzi wake amegundua washambuliaji na mabeki hawakufanya vizuri kwenye mchezo uliopita.

Taarifa za uhakika zimeeleza kuwa Pluijm amewataka washambuliaji hao kuwa makini ili waweze kufunga mabao hasa kipindi cha kwanza dhidi ya Simba.

Pluijm amepanga kutumia mfumo ambao aliutumia kuichinja Simba katika mechi zote mbili za msimu uliopita baada ya kugundua kasoro za beki ya Simba.

Kocha huyo amewatolea macho zaidi washambuliaji hatari wa Simba wakiwemo Mavugo, Ajib na Kichuya ambao wamezifumania nyavu kwenye mechi sita zilizopita, tofauti na Yanga iliyoshinda michezo mitatu, sare mmoja na kufungwa mmoja.

Yanga ilishinda dhidi ya African Lyon mabao 3-0, ikaifunga Majimaji ya Songea 3-0 pia ilishinda 2-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga, ilitoka suluhu na Ndanda FC ya Mtwara kabla ya kufungwa 1-0 na Stand United. Yanga ina pointi 10.

Wakati Simba, ilishinda 3-1 dhidi ya Ndanda FC, ikanyonga 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, ilichanua 4-0 dhidi ya Majimaji, ilishinda 1-0 dhidi ya Azam FC, pia ilitoa dozi ya 2-1 kwa Ruvu Shooting na kutoka suluhu dhidi ya JKT Ruvu.

ZAWADI ZAO

Yanga wameweka siri kubwa kuhusu ahadi zilizotolewa na viongozi wa klabu hiyo ambapo kuna taarifa kuwa huenda wakazoa fedha nyingi kuliko za Simba kama mnyama akichinjwa mbele ya mashabiki 60,000 katika dimba la Taifa.

Mpaka sasa mwanachama maarufu wa Yanga, Catherine Ambakisye ëMama Loraaí ametangaza kununua kila bao kwa shilingi 400,000, pia matajiri wa klabu hiyo jana walitarajiwa kutua visiwani Pemba ili kukutana na wachezaji wa timu hiyo ili kutoa ahadi zao. WACHEZAJI WAPIGWA KUFULI Katika hali isiyo ya kawaida wachezaji wa timu zote mbili za Yanga na Simba wamegoma kuzungumzia mchezo huo, ambapo hatua hiyo imetokana na viongozi wao kuwapiga ‘kufuli mdomoni’.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.