Wabunge, waziri watambiana

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WAKATI zimebaki saa 48 kabla ya kupigwa pambano la Yanga na Simba Jumamosi, mawaziri na wabunge wametoa tambo zao.

Mdau wa soka nchini, Idd Azan ambaye amewahi kuwa meneja wa Simba na mbunge wa jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam, alisema ana imani timu yake itatoa dozi nene kwa watani zao hao wenye maskani yao katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.

Naye Mbunge Kosato Chumi wa jimbo la Mafinga mjini, alisema mwendo wa Simba ni kiboko na wana fursa zaidi ya kutoka kiwanjani kifua mbele.

Mbunge huyo akizungumzia wapinzani wao, Yanga kue- lekea pambano hilo alisema ni wazuri, isipokuwa hali waliyonayo ya kuchoka kutokana na kucheza muda mrefu bila ya kupata mapumziko huenda itawagharimu.

Alisema kuwa wachezaji wa Yanga walishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ya msimu uliopita na baadaye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na muda wote huo hawakupata mapumziko hivyo wazi wana uchovu.

“Ni vyema kama Simba wakatumia vizuri kuchoka kwa watani zao, ili kupata ushindi kwenye mechi hiyo. Kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kuzoa pointi zote tatu muhimu,” alisema Chumi.

Aidha, alisema huu ni msimu wa mwisho kwa Ibrahim Ajib kucheza hapa nyumbani

kwa vile kiwango chake kipo juu sana.

Mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Fumo Felician alisema mechi hiyo itakuwa ngumu sana.

Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani kwa upande wake alisema ana imani Jumamosi Simba analiwa bila ya wasiwasi wowote.

Huku William Ngeleja amesema kuwa safari hii Simba imesajili vizuri na wana imani Yanga hawatoki kwenye mpambano huo.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba Hassan Dalali alisema kuwa hawezi kusema chochote kwa vile hivi sasa ana msiba baada ya kufiwa na mtoto wake mwishoni mwa wiki hapa Dar es Salaam, huku Ibrahim Akilimali akijipiga kifua na kutamka: “Yanga iko nasubiri siku niende uwanjani kuangalia mchezo huo.” WAAMUZI/ VIINGILIO Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka mkoani Morogoro ambaye atasaidiwa na Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha.

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF), limetangaza viingilio katika mchezo huo kuwa ni sh 7,000, 10,000, 20,000 na 30,000.

Hata hivyo, mashabiki watalazimika kuingia kwa tiketi za mfumo wa elektroniki ambao utakuwa wa kwanza kutumika katika mechi hiyo kubwa ya wapinzani wa jadi katika soka nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba (kushoto) akimpa mkono Mama Fatma Karume baada ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la uwanja wa klabu ya Yanga lililopo Kigamboni Dar es Salaam, jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.