Kizimbani kwa wimbo wa kumuudhi JPM

BURUDANI - - HABARI - NA FURAHA OMARY

MSANII Fulgency Mapunda maarufu kwa jina la MwanaCotide (32), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kusambaza wimbo uitwao ‘ Diktekta Uchwara’ kwa lengo kumuudhi Rais Dk. John Magufuli.

MwanaCotide na mtayarishaji wa nyimbo, Mussa Sikabwe (39), wote wakazi wa Dar es Salaam, walifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali, Dereck Mkabatunzi, aliwasomea washitakiwa hao ambao wanatetewa na Wakili Jeremiah Ntobesya, shitaka la kusambaza kupitia mtandao wa YouTube.

Mkabatunzi alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, siku isiyofahamika Agosti, mwaka huu, katika maeneo ya Manzese, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Alidai washitakiwa hao kipindi hicho kwa

kupitia mtandao wa YouTube waliwezesha na kusambaza wimbo uliolenga kumuudhi Rais Dk. Magufuli uliokuwa na jina la ‘Diktekta Uchwara’.

Washitakiwa hao walikana shitaka hilo, ambapo Wakili Mkabatunzi alidai upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Kwa upande wake, Wakili Ntobesya aliomba washitakiwa kupatiwa dhamana, ombi ambalo upande wa jamhuri haukuwa na pingamizi nalo.

Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaotia saini dhamana ya sh. milioni 10 kila mmoja. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Oktoba 12, mwaka huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.