Okwi jezi yako hiyo hapo-Kichuya

BURUDANI - - HABARI - NA NASRA KITANA

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba, Shiza Kichuya amesema kuwa yupo tayari kurejesha jezi namba 25 anayoitumia kwa sasa endapo ataambiwa afanye hivyo.

Kauli hiyo ya Kichuya, imekuja baada ya kuwepo taarifa aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Emmanuel Okwi, atarejeshwa kikosini katika usajili wa dirisha dogo msimu huu na kupewa jezi ambayo alikuwa anaitumia hapo awali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kichuya alisema yupo tayari kuvaa jezi yenye namba yoyote ambayo atapewa na uongozi wa Simba.

Alisema yeye ni mchezaji mwenye uwezo na kama akitokea Okwi akataka kuvaa namba anayovaa sasa, hatakuwa na kinyongo kumvulia kwani anajua wote ni timu moja na wapo kwa ajili ya kuipigania Simba.

“Ninachoangalia mimi ni timu yangu kupata ushindi ‘issue’ (suala) la namba kwangu siyo tatizo kwani mimi nachezea namba yoyote ile inayokuja mbele yangu ama ninayopewa na viongozi wangu,”alisema Kichuya.

Wakati huo huo, kiongozi mmoja wa Simba amesema kuwa watalazimika kumtema mchezaji mmoja wa kigeni ili waweze kupata nafasi ya kumsajili Okwi.

Alisema Wameshakamilisha idadi ya wachezaji wa kigeni hivyo ili kuweza kupata nafasi watamuondoa mchezaji mmoja na nafasi yake itachukuliwa na streka huyo raia wa Uganda.

“Tutasubiria ripoti ya mwalimu (Joseph Omog) atasema nani abaki na nani aondoke lakini lazima tutamuacha mmoja,”alisema

Wachezaji wa kigeni wa Simba ni kipa kutoka Ivory Coast, Vicent Angban, Laudit Mavugo (Burundi), Juuko Murshid (Uganda), Mussa Ndusha ( Congo), Frederic Blagnon (Ivory Coast) na Janvier Bokungu(Congo).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.