MO amwaga mamilioni kwa wachezaji wote

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

MFADHILI wa zamani wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘MO’, amemwaga kitita cha sh. milioni 10 na kuwapa wachezaji wa timu hiyo.

MO alitoa fedha hizo jana ikiwa ni motisha kwa wachezaji wa Simba ambao walicheza kwa jihadi katika mchezo wao dhidi ya Yanga.

Yanga na Simba zilijitupa dimbani katika mchezo namba 49 mzunguko wa saba wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Oktoba Mosi mwaka huu na kutoka sare ya bao 1-1.

Wafungaji walikuwa Amis Tambwe ambaye bao lake lilisababisha tafrani huku Simba wakisawazishia kupitia kwa Shiza Kichuya aliyepiga kona maridadi ambayo ilitinga wavuni moja kwa moja.

Fedha hizo zimetolewa ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu ambao Simba imejiwekea msimu huu ambapo katika kila mechi ambayo timu yao itacheza na kupata matokeo mazuri, wachezaji wanapewa motisha ili kuwapa nguvu ya kujituma zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mfadhili huyo kwenda kwa uongozi wa klabu hiyo, imeelezwa kuwa mfadhili huyo anatambua mchango mkubwa wa wachezaji tangu kuanza msimu huu na juhudi za kutafuta ushindi katika mchezo dhidi ya Yanga.

MO alisema katika mchezo dhidi ya Yanga wachezaji walijituma na kupigana kwa hali na mali kuhakikisha timu yao inashinda, lakini mambo yalikuwa tofauti.

“Kila mtu anajua kilichotokea uwanjani na laiti kama mambo yangeenda sawa tungeibuka na ushindi lakini hata kama hatukupata ushindi wachezaji wetu walijituma, hivyo wanastahili motisha,” alisema MO.

Kabla ya MO kutoa fedha hizo, wanachama mashuhuri, wabunge na waziri ambao ni mashabiki wa Simba waliwapa wachezaji hao sh. milioni 10.

Simba inaoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 17 kibindoni baada ya kushuka dimbani mara saba.

Motisha hiyo inatarajiwa kuongeza kasi kwa Simba kufanya vizuri katika mechi zingine, kwani uongozi wa klabu hiyo umepania kutwaa ubingwa msimu huu.

Mbali ya fedha hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope, wiki iliyopita alitangaza kutoa zawadi ya gari kwa kila mchezaji atakayefanya vyema msimu huu.

Hanspope ameshafanya hivyo kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ambaye amepewa gari aina ya Raum ambalo anatesa nalo kutokana na mchango mzuri aliotoa katika timu hiyo. Kichuya ni mchezaji mwingine anayenyemelea gari pia kutokana na kucheza vyema tangu amejiunga na klabu hiyo msimu huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.