Pluijm akalia kuti kavu

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Yanga, juzi ilikutana kujadili mwenendo wa timu yao na hali inaonyesha kwamba mambo si shwari kwa kocha mkuu, Hans Van Pluijm.

Habari zilizopatikana jana, zimedai kuwa kamati hiyo ilikutana jijini Dar es Salaam, juzi na kugundua kocha huyo raia wa Uholanzi, amekuwa hashauriki.

Pia imeelezwa kuwa siku ya mchezo dhidi ya Simba, uliofanyika mwishoni mwa wiki na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, alishauriwa na viongozi wenzake wa benchi la ufundi ampange kipa Deogratius Munishi’Dida’ inadaiwa kuwa aligoma.

Licha ya jambo hilo, kocha huyo amekuwa akiamua mambo mwenyewe bila ya kusikiliza ushauri kutoka kwa wasaidizi wake, Juma Mwambusi na Juma Pondamali ambao ni makocha wazawa.

Kocha huyopia amedaiwa amekuwa mgumu kufanya mabadiliko hata anapoona mchezaji fulani amechoka, lakini anachukua muda kuamua juu ya jambo hilo.

KUHUSU TIMU KUCHOKA

Kamati hiyo, imegundua kikosi cha Yanga kimekuwa hakipo fiti hasa kipindi cha pili.

Hatua hiyo imetokana na kupitia ripoti ya michezo kadhaa ya gigi kuu Tanzania Bara msimu huu.

Miongoni mwa michezo hiyo ni dhidi ya Stand United ambapo Yanga ilichapwa bao 1-0 katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Pia kwenye mchezo dhidi ya Simba, kipindi cha pili wachezaji wa Yanga walionekana kuchoka na kuruhusu wapinzani wao kusawazisha bao dakika 86, lililofungwa na Shiza Kichuya.

MAZOEZI YAANZA/ KUHAMIA Z’BAR

Kikosi cha Yanga, juzi kilianza mazoezi kwenye uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Polisi Chang’ombe, Dar es Salaam.

Wachezaji wote walifika kwenye mazoezi hayo kwa ajili ya kujiandaa na michezo ijayo ya ligi hiyo.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya kikao hicho, pia kamati hiyo ya Yanga iliyoketi juzi ilimuagiza Kaimu Katibu Mkuu Deusdedit Baraka kuandika barua kwenda Bodi ya kusimamia Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwajulisha kuwa Yanga itatumia uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Hatua hiyo imetokana na uamuzi wa seri- kali kuzuia timu za Simba na Yanga kutumia uwanja wa Taifa baada ya mashabiki kuvunja mageti na viti zaidi ya 1,700.

Serikali inaendelea kufanya tathimini ya uharibifu uliotokea ambapo jana TFF imeipiga faini klabu ya Simba sh milioni 5 kutokana na kitendo hicho.

Jana, Kaimu Katibu huyo wa Yanga, alitua visiwani Zanzibar kwa ajili ya kufuatilia jambo hilo.

KAULI YA BODI YA LIGI

Kufuatia uongozi wa Yanga kutaka kuhamishia michezo yao ya ligi kuu visiwani Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kuu, Ahmed Yahya alisema haiwezekani.

Alisema Yanga haiwezi kuhamia huko kwa vile itakuwa ni kinyume na kanuni za kuendesha ligi hiyo.

“Unajua kila kitu kina taratibu zake, timu inatakiwa kuhamia sehemu iliyopo au kwenye uwanja uliopo karibu na mkoa, sasa kule kuna ligi ya visiwani na utaratibu wake upo, hivyo labda sheria ibadilike,” alisema.

KAMATI YA WAAMUZI YANENA

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama, amesema waamuzi wa bara hawawezi kwenda kuchezesha mechi za ligi kuu visiwani humo.

Alisema huo ni utaratibu wa kanuni hivyo, Yanga kama wameamua kuhamia huko inabidi kanuni zibadilishwe kitu ambacho alisisitiza hakiwezekani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.