BMT yakoromea wapenda madaraka lukuki

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KAIMU Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa ( BMT), Mohammed Kiganja, amesema viongozi wanaoshika nafasi nyingi za kuongoza vyama na klabu za michezo wanazorotesha maendeleo ya michezo nchini.

Akizungumza na BURUDANI, Kiganja alisema amegundua viongozi wanaofanya hivyo ni waroho wa madaraka.

“Iko tofauti sana baadhi ya watu au viongozi wanaotengeneza sheria zao, wanajiwekea vipengele ili kuendelea kuongoza, huku wakienda pia kugombea nafasi mikoani. Sijui watapata muda gani kutekeleza majukumu yao vizuri, “alihoji katibu huyo.

Alisema zipo sheria zinazowakataza viongozi wa vyama mbalimbali, likiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au klabu, kuwania nafasi katika mikoa au klabu.

Aliwataka viongozi wa mikoa kutowapa nafasi viongozi wenye nafasi katika ngazi ya kitaifa kutokana na kile alichodai wakishinda, wanasahau majukumu yao.

Kauli hiyo imekuja baada ya kiongozi huyo, kuulizwa kuhusu kauli yake juu ya mtindo uliozuka hivi sasa kwa baadhi ya viongozi wa TFF, klabu za Simba na Yanga kugombea nafasi mbalimbali katika vyama vya soka vya mikoa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.