Mkataba Yanga una maswali mengi kuliko majibu

BURUDANI - - MBELE - TAFAKARI YA CHIBURA Na Edgar CHIBURA 0714 522408

OKTOBA 6, mwaka huu ilitoka taarifa iliyozagaa katika mitandao ya kijamii inayosadikiwa kutoka Bodi ya Baraza la Wadhamini wa Yanga kwa vyombo vya habari kuhusu mkataba waliodai kuingia na kampuni moja iliyoanzishwa kwa madhumuni ya kufanya biashara na timu ya Yanga.

Mkataba huo wa miaka 10 unasemekana ulitiwa saini na pande hizo mbili Septemba 3, 2016 na utaanza kufanya kazi kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu hadi unasambazwa ni mwezi mmoja umepita na ni miezi miwili tangu wanachama walitoa baraka hizo za ukodishwaji.

Kabla ya kukujuza kilicho ndani ya mkataba na athari zake kwa Yanga siku za usoni, bado kuna maswali mengi juu ya usiri na tahadhari kubwa iliyopo juu ya mkataba huo.

Wakati kikao cha dharura kilichoketi Agosti 6 mwaka huu, japo kilikuwa kinyume cha katiba ya Yanga kwa ibara ya 22 inayosema namna gani mkutano wa dharura unavyoitishwa, kuanzia kifungu cha kwanza mpaka cha tano ni wazi kikao hakikukidhi vigezo vya udharura huo.

Usiri mwingine ni pale ambapo waliwekeana saini ilikuwa kimya kimya, eti kuhofia wapizani wao kuiga, hiki nacho ni kichekesho kweli kama ni jambo zuri lenye maslahi kuigwa ni ufahari, lakini ukitaka usiigwe wakati kila wahusika wana wanachama wao sioni tatizo.

Lengo sio kuigwa ni kuficha aibu ya kile kitakachoonekana machoni mwa watu. Hata hivyo walisubiri hadi itangazwe Yanga imepewa eneo la ujenzi wa uwanja huko Kigamboni, bahati mbaya hatukuona hati ya eneo hilo imekabidhiwa kwa wadhamini wa Yanga au ilikuwa maneno matupu tu!

Sijaona utiaji wa saini katika makabidhiano hayo yote, bali yalikuwa maandalizi ya kutangaza mkataba usioeleweka ulioishia kutupiwa mitandaoni ili wasikilizie joto la wanachama wa Yanga kuwa wanasemaje au wanatakaje.

Ukisoma katiba ya Yanga Ibara ya 25 kuhusu jambo lolote kubwa la kuhitaji maamuzi ya wanachama kifungu (5) kinasema: ìMaamuzi ya mabadiliko yoyote ya makao makuu ya Yanga Africans Sports Club, marekebisho yoyote katika katiba na kanuni na mabadiliko yoyote ya agenda ya mkutano mkuu wa kawaida huhitaji theluthi mbili (2/3) ya kura halali zilizopigwa na wajumbe rasmiî na kura zenyewe ziwe za siri kuhusu jambo hili ambalo ni kubwa la kubadili kanuni na taratibu za uendeshaji wa timu na kabla ya hapo, lazima taratibu zifuate za uitishwaji wa mkutano huo kwa kupeleka agenda kwa wanachama kati ya siku saba hadi 15 zijadiliwe kwa kina, yote hayakufuatwa katika kikao hicho cha Agosti 6, mwaka huu.

Ukiusoma mkataba kwa makini utaona mambo mengi ya kutia shaka sehemu 1:1 ikielezea sababu za ukodishwaji huo ni kukabiliwa na changamoto za fedha katika kuendesha timu, usajili mdogo wa wanachama, mifumo isiyo na ufanisi ya kiutendeshaji, kushindwa kujipatia kipato cha kibiashara katika hatimiliki ya mambo ya kibiashara, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusababisha timu ijiendeshe kwa hasara na kuwa tegemezi.

Haya ni majukumu ya kiongozi kuyaondoa, hakuna uhusiano wa ukodishwaji na mfumo mbovu wa uendeshaji unaofanywa kwa makusudi na viongozi hili wajinufaishe kama sasa wanavyotaka kujikodisha ili wapate faida.

Haya matatizo waliyoyataja wanaweza kuyamaliza pasipokukodisha timu kwa sababu anayekodisha ndiye kiongozi wa juu wa timu mwenye mamlaka, aliyekuwa akiwalipia ada wanachama wake kabla ya kuwa kiongozi badala ya wanachama kujitoa kwa ajili ya timu.

Suala la ada ni kuandaa mfumo mzuri wa ulipiaji, wanachama wapo tayari lakini pia kuwe na uwazi wa matumizi na ada zao. Hizi sio sababu za msingi labda angesema amekwamishwa na nani kutokuchukua hatua zilizosababisha ashindwe na akikodisha atawezaje?

Hata hivyo bado hajaonyesha baada ya miaka 10 hayo matatizo yatakuwa yameondoka vipi? Hajasema timu ataiachia kitu au biashara gani ili ijitegemee.

Katika sehemu ya 3:0 ya mkataba wadhamini wamekubaliana na mkodishaji kampuni ya YANGA YETU atapewa haki zote, majukumu yote, jina na nembo kwa ajili ya kutumika kibiashara bila kuingiliwa katika muda wa mkataba wake.

Hii ndiyo hatari zaidi kwani akifanya vibaya au kuingia mikataba isiyo na maslahi kwa timu hakuna kiongozi au wanachama atakayeuliza au kuhoji. Wanachama wanatakiwa wakae kimya kwa muda wote wa miaka 10.

Kwa maana nyingine hapa kamati tendaji imevunjwa tangu Septemba Mosi, 2016 pale ambapo Bodi ya Baraza la Wadhamini walipoikabidhi timu kwa Kampuni ya Yanga Yetu, kwa sababu hiyo pia hakutakuwa na sababu zozote zile kuwa na uchaguzi kwa muda wa miaka 10 pale ambapo timu itarudishwa kwa wanachama baada ya muda wa ukodishwaji kuisha.

Je, itakabidhiwa kwa uongozi upi? Kama ni bodi ya wadhamini ndiyo watapokea timu na kuiendesha kwa muda huku wakiweka mazingira ya uchaguzi, kwa mujibu wa katiba wanaruhusiwa kujihusisha na uongozi moja kwa moja?

Kama kamati tendaji haina kazi ni nani ataitisha mkutano mkuu wa wanachama ili wakabidhiwe timu? Hakuna kiongozi au mjumbe wa bodi mwenye majibu ya moja kwa moja ya maswali hayo.

Sehemu ya 3:3 inaeleza mkodishwaji atailipia Yanga deni la sh. bilioni 11.676 inayodaiwa kama mmiliki na mkodishwaji moja, hiki nacho ni kitendawili.

Anayedai pesa hizo alishasema kwamba anajitolea na hakuwa anafanya biashara Yanga, hadi kuzuia watu wasihoji mapato na matumizi kwa sababu ni pesa zake za mfukoni huku akiwakataa wadhamini mbalimbali.

Leo anaidai Yanga kupitia kampuni ya Yanga Yetu, mbona hajaweka wazi alikusanya kiasi gani kupitia wadhamini, ada na makato ya uwanjani? Angeweka wazi alipata kiasi gani kwa miaka hiyo yote na namna gani amein- giza timu katika deni lisilolipika huku kukiwa hakuna cha kujivunia kutokana na matumizi ya fedha hizo!

Kama ni wachezaji wa kigeni Yanga haikuanza leo kuwaleta walikuwepo kina Nonda Shabani ‘Papii’, Ramazani Waso, Costantine Kimanda na wengeneo, haikuwa mara ya kwanza timu kuweka kambi nje ya nchi kwani waliwahi kwenda Brazil mwezi mzima kama ni makocha wa kigeni walikuwepo mfano, marehemu Tambwe Leya lakini hakuna kiongozi aliyeacha deni lisilolipika na kubwa kiasi hicho.

Kwanza kabla ya kulipia hilo deni ni bora arudi kwa wanachama wasomewe mapato na matumizi kwa mujibu wa katiba yao ibara ya 19 kifungu cha 3:4 kuhusu mamlaka na kazi za mkutano mkuu wa wanachama.

Bado sehemu ya tatu kifungu cha 2:3 cha mkataba, kinasema mkodishwa atailipa Yanga milioni 100 kuimarisha matawi. Wakati hili sio tatizo milioni 100 kila mwaka kuimarisha matawi nani kasema yamelegalega na katika lipi wao wanahitaji mataji tu, na yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) aidha Kombe la shirikisho au klabu bingwa Afrika ndiyo shida yao si pesa za kuwapa.

Hii nayo ni janja ya kuwazuia wanachama kuhoji kuhusu mkataba huu. Faida itakayopatikana itakayothibitishwa na kampuni ya Yanga Yetu si uongozi itatoa asil- imia 25 kwa timu ambayo kimsingi ipo chini ya mkodishwaji ajenge viwanja kitu ambacho hakipo kama waliendesha kibiashara na kubakiwa na deni la karibu sh bilioni 12 ila wakikodisha pamoja na kulipa deni hilo faida itakuwepo?

Hapo hapo sehemu ya 4:0, mkodishwaji atalipa hasara katika mkataba kutoka mfukoni mwake bila kudai fidia je mkataba gani huo unajadili hasara tu?, wakati hakuna biashara ya aina hiyo popote duniani.

Haikuishia hapo sehemu ya 3:14, Yanga watafuatilia wadai wake wote kabla ya ufanisi wa mkataba huu kuanza. Hapa napo ni kiini macho, bado uongozi haujatuambia kwanini pesa hizo walizikataa na sababu ya kufanya hivyo haijaondolewa, leo wanazichukua wataalamu na mikataba wanaoona kuzikataa fedha za wadhamini ilikuwa Yanga ionekane inasaidiwa na mkodishwaji tu ili aweze kuikodi kirahisi lengo amefanikiwa baada ya kupewa timu bure inadaiwa ameenda kuchukua chake TFF.

Nawasihi Watanzania hakuna bure ya masharti hapo ni biashara anafanya ingawa si vibaya, ni vyema kungekuwa na uwazi tangu mwanzo ili yawekwe mazingira bora ya kibiashara kuliko kujificha kwenye kivuli cha ufadhili.

Naipongeza serikali kuingilia kati jambo hili utaratibu ufuate na kukidhi vipengele vya katiba 3:15 inasema mkataba ukifika ukomo, Yanga Yetu itakuwa na haki kurejesha kile ilichokikodisha kwa maana ya timu, jina na nembo hapa maendeleo yako wapi?

Viwanja vipo wapi? Na utegemezi utakuwa umeondoka? Haya yote yanaonyesha ni mkataba wa kijanja watu/ mtu apige pesa aishie zake hakuna cha zaidi. 4:3 inafafanua kwamba mkataba ukivunjika kwa sababu zozote zile mkodishwaji alipwe fidia ya hasara zote za nyuma, likiwemo deni la bilioni 12.

Najua wana Yanga wana kiu ya maendeleo lakini hii isiwafanye kuwa wanyonge kiasi hicho kuzuia uwezo wa kifikiria. Kila mwanachama au Mtanzania anahitaji muwekezaji au ukodishwaji wenye maslahi kwa timu kimaendeleo kwa ujenzi wa miundombinu na vitega uchumi na si vingenevyo. Tuonane wiki ijayo kwa tafakari zaidi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.