Chirwa atoa gundu

BURUDANI - - HABARI - NA VICTOR MKUMBO

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Obren Chirwa, ametoa mkosi, baada ya kufunga bao lake la kwanza katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Chirwa sasa anaungana na kiungo wa Manchester United, Paul Pogba ambaye alifunga bao la kutoa nuksi dhidi ya Leicester City katika mchezo wa ligi kuu ya England hivi karibuni.

Jana, Yanga ilipata pointi tatu baada ya kuilaza Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchezaji huyo raia wa Zambia, alikuwa na hali ngumu tangu alipojiunga na Yanga kabla ya jana kuwainua jukwaani mashabiki wa klabu hiyo kwa bao la dakika ya 44.

Chirwa, aliyekuwa akicheza pacha na Amis Tambwe, alifunga bao hilo kwa shuti kali akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Simon Msuva.

Awali, beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul, alipanda mbele kusaidia mashambulizi dakika ya kwanza, lakini shuti lake lilipaa langoni.

Dakika mbili baadaye Chirwa, alifanya shambulizi la kushitukiza na kiungo wa pembeni, Deus Kaseke, alipiga shuti nje.

Kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe, Thabani Kamusoko, alipiga shuti la mbali lililotua miguuni mwa mabeki wa Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa pembeni wa Mtibwa, Haruna Chanongo, nusura afunge bao dakika ya 32 kabla ya shuti lake kutoka nje.

Yanga iliongeza kasi ya mchezo na dakika ya 35 beki wa kushoto, Haji Mwinyi, alifumua shuti lililopanguliwa na kipa wa Mtibwa, Benedict Tinoco.

Mtibwa ilisimama imara kwa kulisakama lango la Yanga kama nyuki na dakika ya 41 Ibrahim Rajabu, alipiga mkwaju nje.

Kipindi cha pili Yanga ilifanya shambulizi zito dakika ya 55 kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Geofrey Mwashiuya, uliodakwa na kipa wa Mtibwa, Tinoco.

Mtibwa ilifanya shambulizi la kushitukiza dakika ya 63 na kupata bao la kusawazisha lililofungwa kwa shuti na Chanongo, baada ya kupata pasi ya Salim Mbonde.

Yanga ilipata bao la pili lililowekwa kimiani na Msuva dakika ya 68 akiwa ndani ya eneo la hatari, baada ya mabeki wa Mtibwa kushindwa kuokoa.

Mchezaji wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma, alifunga bao la tatu dakika ya 79 akiunganisha pasi ya Mwashiuya.

Yanga: Deo Munishi, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Vincent Andrew, Kelvin Yondani, Juma Makapu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Amiss Tambwe na Deus Kaseke.

Mtibwa: Benidict Tinoco, Rogers Gabriel, Issa Rashid, Kassim Ponera, Dickson Daudi, Shabani Nditi, Ali Makalani, Mohammed Issa, Rashid Mandawa, Ibrahim Rajabu na Haruna Chanongo. Azam mwaka wa tabu Katika ligi hiyo jana, Mbao FC iliichapa Toto African mabao 3-1, Majimaji ilizamishwa 1-0 na Kagera Sugar, mjini Shinyanga Azam iliendelea na kuwa mwaka wa tabu baada ya kulambwa 1-0 na Stand United, JKT Ruvu na Prisons zilitoka suluhu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.