Mtibwa bado kuwa kama Yanga SC

BURUDANI - - HABARI - NA ATHANAS KAZIGE

MRATIBU wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser, amesema bado bodi ya timu hiyo haijaamua jinsi gani wataweza kuingia katika mfumo wa hisa ili kupata maendeleo zaidi ya soka.

Hadi sasa Yanga imekuwa ya kwanza kutangaza kwamba imeikodisha klabu hiyo kwa Kampuni ya Yanga Yetu, ambayo imesaini mkataba wa miaka 10 na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, lakini upande wa Mtibwa wao bado wanakuna kichwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Bayser alisema bodi hiyo kila mara ikipanga kukutana, kunaibuka ratiba zingine zinazosababisha waahirishe mjadala huo.

Alisema azma ya kuingia katika mfumo wa hisa upo pale pale, lakini mpaka siku watakapokutana viongozi wote wa klabu hiyo yenye makazi yake huko Turiani mkoani Morogoro, kujadili suala hilo na kupitishwa kwa kauli moja.

Alisema lengo la kufanya mabadiliko ni kutaka kuhakikisha wanajenga uwezo wa kuendesha timu yao ili iweze kwenda na wakati kwa kuwa na vyanzo vingi vya mapato kuliko kutegemea chanzo kimoja cha kiwanda cha sukari cha Mtibwa.

Aliongeza kwamba, bodi hiyo ikikutana itaweza kuangalia uwezekano wa kutengeneza uwanja mpya wa kisasa eneo la karibu zaidi na makazi ya mashabiki wa timu hiyo tofauti na uliopo hivi sasa.

“Tuna mipango mizuri ya kuendeleza klabu yetu, jambo la msingi ni kuhakikisha tunajenga uwanja na kuimarisha vyanzo vya timu ili kuondokana na utegemezi, lakini hisa lazima tukae chini tuone nini cha kufanya kabla ya kufikia uamuzi sahihi,”alisema Bayser.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.