Isihaka: Nashukuru nimetulia African Lyon

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

NAHODHA wa zamani wa Simba, Hassan Isihaka, amesema kuwa hivi sasa ametulia baada ya kuondoka Msimbazi ambapo amedai alishindwa kufanya vizuri kutokana na kupigwa zengwe kila kukicha.

Akizungumza na BURUDANI hivi karibuni, mchezaji huyo alisema kuwa kitendo cha kupelekwa kwa mkopo kucheza African Lyon, kimempa faraja kwani ana uhuru mkubwa wa kujifua zaidi ili kuhakikisha kiwango chake kinapanda.

Alisema toka ametua Lyon amegundua kiwango chake kimepanda na anaendelea kujifua kwa nguvu zote huku akiwasilikiza kwa makini makocha wake kila wanapomfundisha.

“Unajua pale Simba kuna mambo mengi nyuma ya pazia, kila kukicha kunazuka mambo kibao, lakini kwa sasa nipo huru naendelea na mazoezi ya nguvu na unaona nafanya vizuri tofauti na nilipokuwa Simba,” alisema Isihaka.

Alisema kuwa yupo tayari kurudi Simba kama watamhitaji ingawa ametaka iwe kwa mazungumzo mapya, huku akiweka wazi lengo lake kwa sasa ni kucheza soka nje ya nchi ili kujiongezea kipato.

“Milango kwangu iko wazi kwa timu yoyote, lakini nina imani kwamba nitapata timu ya kwenda kufanya majaribio nje ya nchi, lakini nina kila sababu ya kuongeza bidii ili niweze kuwa katika kiwango cha juu,” alisema nahodha huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.