Akilimali: Utazuka mgogoro mzito

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KATIBU wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutokubali klabu hiyo kukodishwana kudai utazuka mgogoro mzito endapo mpango huo utatekelezwa.

Kauli ya Akilimali imekuja wakati zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika mkutano wa dharura wa klabu hiyo ili kutoa ridhaa ya kukodishwa kwa miaka 10 kwa Mwenyekiti wake Yusuf Manji.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, katika Ukumbi wa Idara (MAELEZO), akiwa ameambatana na baadhi ya wazee wa klabu hiyo, Akilimali alisema haiwezekani Manji kukodi klabu hiyo wakati mchakato wake haujafuata taratibu huku ukiwa na sintofahamu nyingi.

Akilimali alisema kitendo cha Manji kulazimisha kukodi klabu na nembo yake kitaipeleka klabu hiyo kwenye vurugu kubwa kuzidi hata ile ambayo ilishawahi kutokea kipindi cha nyuma kwani atawagawa wanachama pamoja na mashabiki wanaotaka mfumo huo na wasiotaka mfumo huo pia.

Alisema wanachama wa Yanga hawataki tena kurudi ambapo walikuwepo mwaka 2002 hivyo ni bora waendelee na utaratibu ambao wameuzoea tangu ilivyoanzishwa klabu hiyo.

“Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya shughuli na kama kuna mtu analazimisha hilo, klabu yetu itaingia kwenye mgogoro mkubwa ambao mwafaka wake hautapatikana kirahisi,” alisema Akilimali.

Naye aliyekuwa mwenyekiti wa matawi ya Yanga jijini Dar es salaam, Mohammed Msumi, alisema kama Manji anataka kuwa na timu ni vyema akaanzisha yake na kuiacha Yanga ijiendeshe kwa mfumo wa kisasa.

“Kuna haja ya kujiuliza maswali mengi mojawapo likiwa ni kwanini Manji anataka mchakato huu ufanyike haraka wakati alishawahi kusema kuwa Yanga inajiendesha kwa hasara? alihoji Msumi.

Msumi alisema kama Manji hawezi kufuata katiba anazo fedha nyingi ambazo anaweza kuanzisha klabu yake bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.