THIS IS OKWI

AANZA LIGI KWA KUPIGA MABAO 4, SIMBA IKIIUA RUVU SHOOTING

Dimba - - Mbele - NA CLARA ALPHONCE

BABA mwenye nyumba ameanza kazi. Hivyo ndivyo unavyoweza kumwelezea Straika wa Simba Mganda, Emmanuel Okwi, baada ya kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 7-0 wakati kikosi chake kilipowafunga maafande wa Ruvu Shooting, katika mchezo uliochezwa jana katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mashabiki wa Simba walipagawa katika mchezo huo wajishtukia wakicha wimbo wao wa kawaida wenye maneno ‘This is Simba’ na kujikuta wakiimba ‘This is Okwi’.

Simba iliyotoka kwenye furaha ya kuwafunga watani wao wa Jadi katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Jumatano iliyopita, jana iliweza kuwazamisha maafande hao katika mchezo ulioonekana kuanza kwa ushindani, lakini baadaye kuwa wa ushindi wa upande mmoja.

Okwi alianza kufungua karamu ya mabao katika dakika ya 18 akiunganisha pasi ndefu aliyopenyezewa na Mzamiru Yassin, kisha akaongeza bao jingine kunako dakika ya 22, akiwalamba chenga mabeki wa Ruvu Shooting na kufunga kirahisi.

Kudhihirisha kwamba yupo kikazi zaidi, aliipatia Simba bao la tatu katika dakika ya 35 kutokana na pasi maridhawa ya Mzamiru kabla ya Shiza Kichuya, kufunga bao la nne dakika ya 42 kutokana na pasi nzuri ya Erasto Nyoni, ndipo Juma Luizio akafunga bao la tano akipokea pasi kutoka kwa Nyoni dakika ya 44 na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 5-0.

Kudhihirisha kwamba amekuja Simba kikazi zaidi, Okwi aliipatia Simba bao la sita katika dakika ya 51, kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Said Ndemla, kutoka winga ya kulia na karamu hiyo ya mabao ilihitimishwa na Erasto Nyoni aliyefungwa dakika ya 82 na kuifanya Simba kutoka uwanjani wakiwa na mabao 7-0.

Mabao hayo manne aliyoyafunga Okwi, yameendelea kumuweka matawi ya juu hapa nchini kwani katika misimu yote aliyocheza, alikuwa mwiba mchungu kwa timu pinzani ambapo mwenyewe amesema hizo ni salamu tu mambo mazuri yanakuja.

Okwi alijiunga na Simba mwaka 2010 akitokea SC Villa ya Uganda, ambapo aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2013 alipouzwa katika klabu ya Etoile du Sahel ya nchini Tunisia, ambapo alicheza msimu mmoja na kuamua kuvunja mkataba baada ya kuchoshwa na kusugulishwa benchi.

Alirudi kwao Uganda na kujiunga na timu yake ya zamani ya SC Villa na baadaye kujiunga na Yanga msimu wa 2013/14, ambapo hakumaliza msimu kwani alicheza mzunguko wa kwanza kutokana na kutofautiana na uongozi kuhusu suala la malipo yake ndipo akarejea Simba na kuichezea msimu wa 2014/15 na kisha akauzwa nchini Denmark katika klabu ya Sonderjyske kuanzia msimu wa 2015/17.

Aliamua kurejea SC Villa ya Uganda baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na timu hiyo ya nchini Denmark, baada ya kuchoshwa na maisha katika timu hiyo na sasa amerejea tena Simba, klabu ambayo mwenyewe amekiri kwamba anaipenda kutoka moyoni.

Msimu wake huo wa mwisho kuichezea Simba kabla ya kutimkia nchini Denmark, alifunga bao moja maridadi dhidi ya Yanga akiwa umbali mrefu, akamchungulia Ally Mustafa ‘Barthez’, akaachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni na Wekundu hao wa Msimbazi wakaondoka na ushindi wa bao 1-0, mchezo uliochezwa Machi 8, mwaka 2015.

Mganda huyo anakumbukwa sana hasa baada ya kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, mchezo uliochezwa Septemba 11, mwaka 2012, akifunga mawili na mengine yakifungwa na marehemu Patrick Mafisango, Felix Sunzu pamoja na aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Juma Kaseja. Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na Aishi Manula, Ally Shomary, Erasto Nyoni, Method Mwanjale/Juuko, Salum Mbonde,James Kotei, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin/Ndemla, Juma Liuzio, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima/Mohamed Ibrahim.

Kikosi cha Ruvu Shooting kiliwakilishwa na Bidii Hussein, Said Imani Madega/Aman George, Yusuph Innocent, Shaibu Nayopa, Mangasin Mangasin, Baraka Mtuwi, Chande Magoja/Said Dilunga, Shaban Msaja, Juma Said, Jamal Mtegeta na Khamis Mussa.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana, Mwadui FC waliifunga Singida mabao 2-1 katika Uwanja wa Mwadui Complex, Mtibwa Sugar ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United, Ndanda FC wakakubali kichapo cha bao 1-0 toka kwa Azam.

Mbeya City wakiwa katika Uwanja wao wa Sokoine jijini Mbeya, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji ya Songea, huku Tanzania Prisons wakiilaza Njombe Mji kwa jumla ya mabao 2-1. Mbao FC imepata ushindi mwembamba dhidi ya Kagera Sugar, wakiicharaza bao 1-0 katika mchezo uliopigwa nyumbani kwao, Uwanja wa Kaitaba.

PICHA KUBWA: Okwi akipongezwa na Erasto Nyoni.

Straika wa Simba, Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kufunga mabao manne dhidi ya Ruvu Shooting jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.