ROONEY, UAMUZI SAHIHI KWAKE NA KWETU PIA

Dimba - - Jumapili -

NDIO, Wayne Rooney angeweza kusubiri kidogo. Gareth Southgate alisharudisha imani juu yake, angemuita tena kikosini. Angeweza kusubiri kuivunja na rekodi ya Peter Shilton kwa kucheza michezo mingi.

Angesubiri pia kuongeza rekodi yake ya mabao. Angeweza kufanya kila kitu kama angeamua kusubiri kidogo na kustaafu baadae.

Lakini bahati mbaya Rooney hakutaka kufanya tunavyotaka. Hakupanga kuondoka kwa kishindo hiko. Kichwani mwake alishakuwa na njia yake nzuri ya kuimaliza safari yake.

Safari ya miaka 14, akiwa na jezi ya taifa la England, ameimaliza kiume. Kiume kweli kweli!

Mwaka mmoja kabla ya fainali za kombe la dunia kule Russia, Wazza anasimama na kutundika daluga. Ni wachezaji wangapi unaowajua duniani wenye ujasiri wa aina hii?

Samuel Etoío aliivizia kwanza World Cup, ndio akatundika daluga. Miroslav klose alifanya hivyo pia, alipocheza mwaka 2014, mwezi mmoja baadae akastaafuu. Kila wachezaji ana ndoto ya kucheza Kombe la dunia.

Kwa Baba Kai, hadithi ni tofauti kidogo. Safari ya Urusi haikuwa na maana kubwa kwake kuliko maamuzi aliyoyachukua.

Ana mechi 199 za England kwenye wasifu wake, ndiye mchezaji wa pili aliyecheza michezo mingi zaidi. Ana mabao 53, ndiye mfungaji bora wa muda wote wa England.

Rooney angehitaji nini zaidi? Imetosha sasa. Imetosha kwake na kwetu pia.

Hakutaka kuitwa kikosini na kwenda kuishi maisha ya majaribu kambini. Maisha ya kutumika kama spea tairi, Rooney hakupendahili limtokee tena.

Anahitaji kukumbukwa kama nyota wa England. Mchezaji bora wa muda wote! Binadamu yule mwenye uwezo wa kupindua ubao wa matokeo muda wowote atakao. Rooney amechagua heshima hiyo.

Ni fedheha kwake kuendelea kuvaa jezi ya England na kushuhudia taifa lake likiteswa na timu kama Iceland. Timu aliyoiangamika kwa guu lake mwaka 2004, pale City of Manchester.

Huu si wakati wa yeye kukaa benchi na kuwashuhudia madogo kama Rashford na Lingard wakiruka ruka tu uwanjani.

Bora apumzike, angekuwa mjinga kama angejaribu kutaka kushindana na wakati. Huu si wakati wake tena.

Anajua ubora alioubakiza kwenye miguu yake, kwanini ajilazimishe kuubeba mzigo asioweza kujitwisha? Hana analoweza kufanya kwa England tena.

Ni bora aumie akiwa kwenye Tv nyumbani kama wanavyoumia mashabiki wengine wa England. Kwenda Russia, ingekuwa kamari kubwa sana maishani mwake.

Katika nyakati zake bora uwanjani, ameishia kupata bao moja tu kwenye Kombe la dunia. ingehitaji akili ya kiuwendawazimu kumuaminisha kuwa angeweza kufanya maajabu zaidi kule Urusi.

Acha apumzike. Acha jina lake libaki nyuma ya kina Sir Bobby Charlton, Sir Geoff Hurst, Bryan Robson, Gary Lineker na Shilton. Huu ndio mwisho sahihi kwake.

Usain Bolt anaijutia kamari aliyoicheza kwa kukubali kukimbia London Marathon, mwaka huu. Mo Farah vile vile, kwanini Rooney aiweke majaribuni heshima yake? Pumzika Baba Kai.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.