Arsenal ilianzishwa mwaka gani?

Dimba - - Jumapili -

SWALI: Naitwa Ezekiel wa Makuyuni, naomba kujua klabu ya Arsenal ilianzishwa mwaka gani na kocha wake wa kwanza alikuwa anaitwa nani? 0763122202.

JIBU: Klabu ya Arsenal ilianzishwa rasmi mwaka 1886 na wafanyakazi wa Kiwanda cha silaha Woolwich, baadaye Kent na saasa wamehamia Kusini Mashariki mwa Jiji la London. Baadaye iliamua kubadilika na kuwa klabu ya kulipwa mwaka 1891 na kisha kujiunga na Ligi ya England miaka miwili baadaye.

Makocha wa kwanza wa klabu hiyo hawakuwa wakijulikana sana ila Thomas Mitchell, raia wa Scotland ndiye aliyekuwa kocha wa kwanza rasmi kuanza kuinoa timu hiyo kwa mkataba kuanzia Machi 1897 hadi Machi 1898.

SWALI: Pole na majukumu ndugu mhariri, naomba unitajie kikosi cha Liverpool kilichoishangaza dunia 2002 na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya AC Milan. Naitwa Medico Sanga wa Dar es Salaam.

JIBU: Kwanza nikusahihishe kwamba Liverpool haikutwaa taji la ubingwa wa Ulaya mwaka 2002, bali ilifanya hivyo mwaka 2005 mbele ya AC Milan katika fainali iliyopigwa katika Dimba la Olympic stadium, Istanbul Uturuki, ambapo Liverpool iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 kwa sare ya mabao 3-3.

Kikosi cha Liverpool kilichocheza siku hiyo kilikuwa: Jerzy Dudek, Steve Finnan/Dietmar Hamann, Djimi Traore, Jamie Carragher, Sami Hyypia, Xabi Alonso, Luis García, Steven Gerrard (nahodha), Milan Baros/Djibril Cisse, Harry Kewell/Vladimir Smicer na John Arne Riise.

SWALI: Naitwa Rashid Hamisi Nyangala wa Pugu Kinyamwezi, swali langu naomba unitajie kikosi kilichoitoa Zamalek ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003. 0713999551.

JIBU: Baadhi ya wachezaji waliokuwemo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Juma Kaseja, Said Sued 'Panucci', Ramadhani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Selemani Matola (nahodha), Ulimboka Mwakingwe, Christopher Alex, Emmanuel Gabriel, Yusuf Macho 'Musso' na Athumani Machuppa.

SWALI: Naitwa Anthony Fanuel Lechilema kutoka Mseta, Kongwa, naomba kuuliza mimi ni shabiki mkubwa wa Yanga lakini kwanini timu kubwa haina uwanja wake yenyewe, viongozi hawaoni aibu? 0623352099.

JIBU: Ahsante kwa swali lako, lakini unapaswa kufahamu kwamba, Yanga inao uwanja wake wa Kaunda ambao ungeweza kuboreshwa kwa ajili ya timu kufanyia mazoezi au kuchezea mechi ndogondogo. Hata hivyo, bado uongozi wa klabu hiyo unapaswa kukabiliana na changamoto kubwa ya uwanja mkubwa zaidi ambao klabu hiyo itakuwa ikiutumia katika mechi za ligi na zile za kimataifa.

SWALI: Naitwa Hussein Bakari, niko Muheza Tanga. Naomba mnikumbushe kikosi cha Simba kilichoifunga Yanga bao 5-0 mwaka 2012. 0656500096.

JIBU: Kikosi cha Simba kilichoifunga Yanga 5-0 Mei 6, 2012 kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud 'Chollo,' AmirMaftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/ Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.

SWALI: Wachezaji wawili wa zamani wa Yanga, Nonda Shaaban na Costantine Kimanda, wako wapi hivi sasa na wanafanya nini? Ameuliza msomaji mwenye simu namba 0621880181.

JIBU: Baada ya kutoka Yanga, Nonda alikwenda kucheza kwa mafanikio katika klabu za Vaal Professionals ya Afrika Kusini, FC Zürich ya Uswisi, Rennes ya Ufaransa, Monaco (Ufaransa), AS Roma ya Italia na baadaye kwa mkopo katika klabu ya Blackburn Rovers, kisha akamalizia soka lake katika klabu ya Galatasaray ya Uturuki mwaka 2010. Baada ya hapo alifanya kazi ya kuwa wakala wa wanasoka wa Afrika, kabla ya kurejea kwao Congo DR, anakoendesha biashara ya hoteli kubwa kubwa za kitalii.

Kwa upande wake Kimanda, baada ya kuondoka Yanga aliyoitumikia kwa miezi tisa tu kuanzia Januari hadi Septemba mwaka 1994, alitimkia Uarabuni kukipiga katika klabu ya Sharjah FC ya huko, lakini baadaye akahamia nchini Ubelgiji ambako anafanya kazi katika idara ya ustawi wa jamii jijini Brussels na ameoa mke kutoka kwao Burundi anayeitwa Veronica, mwenye watoto wanne; Monica (10), Yasser (8), Rami (5) na Amel (1).

SWALI: Naitwa Steven John, msomaji wa gazeti la DIMBA kutoka Kibaha, napenda kuuliza ni mwaka gani mashabiki wa Liverpool walipokufa uwanjani na kwa sababu gani? 0783622377.

JIBU: Maafa hayo yalitokea mwaka 1989, wakati mashabiki 96 wa Liverpool walipofariki Uwanjani Hillsborough, kwenye mechi ya Nusu Fainali ya FA Cup kati ya Liverpool na Nottingham Forest, baada ya msongamano na mkanyagano.

SWALI: Nauliza yuko wapi mchezaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ujerumani, Michael Ballack? Na je, anajihusisha na nini kwa sasa? Naitwa Pius Urio wa Kihonda, Morogoro. 0673114281.

JIBU: Michael Ballack alistaafu rasmi soka mwaka 2012, baada ya kuchezea kwa miaka miwili klabu yake ya zamani ya Leverkusen.

Baada ya hapo alikuwa akijihusisha na shughuli ya utangazaji katika runinga mbalimbali, zikiwemo BBC na Sky Sports. Pia amekuwa akifanya kazi ya uchambuzi wa soka katika mtandao wa ESPN.

SWALI: Naomba unitajie kikosi cha Yanga kilichochukua ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwa mara ya kwanza mwaka 1993 jijini Kampala, Uganda. Ni Agustino Kyando wa Mbeya, Airport ya zamani. 062080014.

JIBU: Baadhi ya wachezaji wa Yanga waliotwaa taji la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati walikuwa ni Stephen Nemes, Riffat Said, Mwanamtwa Kihwelu, Ken Mkapa, Willy Martine, Willy Mtendamema, Method Mogella, Salum Kabunda 'Ninja,' Issa Athumani, Zamoyoni Mogella, Hamis Gaga, Stephen Musa, Aboubakar Salum 'Sure Boy', Said Mwamba 'Kizota,' Mohammed Hussein Daima 'Chinga One' na Edibily Lunyamila.

SWALI: Naitwa Magongo wa Magongo; msomaji mzuri wa gazeti la DIMBA. Swali langu, naomba kuuliza hivi, Misri imewahi kuiwakilisha Afrika mara ngapi katika fainali za Kombe la Dunia?

JIBU: Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, Misri imewahi kuiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia mara mbili tu katika miaka ya 1934 na 1990 na kuishia kwenye hatua ya makundi.

Wenger

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.