Zama na kukinukisha hichooo!

Dimba - - Jumapili -

TUMEANZA kusikia mambo yakirindima katika viwanja mbalimbali vinavyochezewa mchezo wa soka, ikimaanisha kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, jana.

Wengi tunafurahia kipindi hiki ambacho kinatuwezesha kuona nani amepanda na kuvuna nini.

Nauogopa sana wakati huu, kwa sababu umejigawa katika makundi mawili; ya machozi ya furaha na ya machungu.

Mfano kati ya timu 16 zitakazochuana kugombea uvingwa huo wa Bongo, sijaona ambayo kwa asilimia zote zimehusisha makocha katika usajili, lakini nina hakika isiyo na shaka kwamba kapu ya mafanikio limebebwa nao.

Nawahurumia makocha kupita kiasi kwa sababu najua misalaba iliyopo mbele yao, haiwahusu ila itawabana.

Kama haitoshi nazifikiria hasira kwa waliotoa fedha zao wakasajili kwa mbwembwe kumbe wakiingia mkenge, kwani utapeli hata kwa wachezaji siku hizi umeota mizizi.

Nafahamu pasi shaka kuwepo kwa makundi ya wachezaji wanaoishi kwa kutegemea usajili katika klabu mbalimbali za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakicheza Kenya ligi na ikitokea labda wameshuka kiwango au kupata majeraha, wanachofanya ni kukimbilia nchi nyingine kutafuta timu.

Ndiyo maana ipo siri kubwa inayowasumbua baadhi ya wadau wa soka hapa nchini, wakijuliza kwanini baadhi ya wachezaji wanafanya vibaya hapa nchini, lakini wakirudi katika timu zao wanakuwa wafungaji bora au mabeki wa kusifika au viungo hodari.

Hawa hawatambui kwamba zipo ligi za nchi zinazofanywa ni kwa ajili ya kuuguzia majeraha na pindi wakishapona wanarejea katika maeneo wanayotaka kucheza na ili kulinda majina yao wanajitahidi kufanya vizuri.

Hizi ndizo tabia za baadhi ya wachezaji ambazo pamoja na mambo mengine pia zimewahi kuwafanya makocha wakatimuliwa kutokana na kutojua utapeli huu.

Lakini yote haya, kila tunavyopiga kelele tukitaka makocha tuhusishwe kwa asilimia zote katika usajili inakuwa ni kelele za mlango.

Kwa hiyo kila inapofikia wakati huu, ndipo kumbukumbu za aina hii zinaporejea, kwani kama mchezaji na kocha niliyehudumu katika soka kwa kipindi kirefu kuyaona haya kwangu haihitaji miwani.

Nimeshaona wachezaji waliochukua fedha wakasajili ilihali wagonjwa, nina idadi kubwa tu ya wachezaji majeruhi, lakini wamepona kiasi na hata wapo walioshuka viwango kiasi cha kuachwa na timu zao, lakini kwetu wakaonekana kivuno, kama alivyoona Chungu kuokota ganda la mua la jana.

Nakihesabu kipindi hiki kuwa ni kigumu sana kwa makocha, lakini chenye faraja kwa wachezaji hasa wapya watakaojitahidi kuonyesha vipaji vyao ili kuweza kujitengenezea maisha mazuri ya baadaye. Kila la heri Ligi Kuu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.