TAMBWE, TSHISHIMBI NI VITA MPYA YANGA

Dimba - - Mbele - NA CLARA ALPHONCE

KITENDO cha Straika wa Yanga, Amis Tambwe, kurejea kikosini kuungana na kiungo, Papy Tshishimbi, kinatarajiwa kuongeza chachu ya ushindi kwa Wanajangwani hao katika safu yao na kuondokana na mapungufu yaliyoonekana katika eneo hilo katika katika mechi yake dhidi ya Yanga.

Yanga wanashuka dimbani leo kuwavaa wageni wa Ligi Kuu, Lipuli FC ya mkoani Iringa inayonolewa na kocha mzawa Selemani Matola.

Kutokana na kombinesheni ya wachezaji hao, bila shaka itakuwa ni vita nyingine kwa timu zitakazokutana na kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Uwepo wa Tambwe katika kikosi cha Yanga, kuna nafasi kubwa za kuisadia timu yake hiyo kuibuka kidedea ukizingatia shughuli pevu inayofanywa na kiungo fundi Mkongo Tshishimbi, aliyeanza kujizolea sifa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini.

Ubora wa Tshishimbi kupiga pasi murua, kwenda mbele na kutengeneza mashambulizi huku akishirikiana na kiungo Thaban Kamusoko, kunatajwa kuwa ni nafasi nzuri ya kumwezesha Tambwe kuonyesha uwezo wake wa kupachika mabao.

Wanajangwani hao walikosa mtu kama Tambwe kwenye safu ya ushambuliaji kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambapo Donald Ngoma ambaye hakuwa fiti sambamba na Ibrahim Ajib, walishindwa kutumia vema nafasi kadhaa walizowekewa na Tshishimbi na Kamusoko kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, shughuli hiyo inaweza kuwa pevu kutokana na ahadi ya kocha wa Lipuli, Seleman Matola aliyeionya Yanga na kuitaka isitarajie mteremko kwa vile timu yake pia inahitaji pointi tatu ili ijiweke vizuri katika msimamo wa ligi hiyo.

Matola aliliambia DIMBA kwamba, kikosi chake kimeiva na anaamini kitakuwa tishio katika michuano hiyo, licha ya matarajio ya wengi kwamba ugeni wao katika ligi unaweza kuwafanya wafungwe kirahisi.

Naye Kocha wa Yanga, George Lwandamina, alikiri kuwapo na mapungufu kwenye safu ya ushambuliaji ambapo alisema majeraha ya Tambwe na Obrey Chirwa yaliwagharimu katika safu ya ushambuliaji.

“Kurejea kwa Tambwe ni jambo jema kwetu, itatusaidia sana ukizingatia mchezo uliopita huduma yake ilikuwa ni muhimu pale mbele, ambapo kulikuwa na mapungufu kadhaa lakini simaanishi waliokuwapo walicheza vibaya,” alisema.

Kuna asilimia kubwa mchezo wa leo Tambwe kuongoza mashambuliaji sambamba na Donald Ngoma ambao upacha wao utaongezewa nguvu na kiungo Tshishimbi na kulifanya pambano hilo kuwa la vuta nikuvute.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.