Umesikia sarakasi za Chirwa Yanga

Dimba - - Jumapili - NA CLARA ALPHONCE

HATIMA ya mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa na winga Deusi Kaseke wa Singida United, sasa itajulikana wiki ijayo.

Wachezaji ambao wamesimamishwa kutokana na kosa la kumsukuma mwamuzi katika mechi ya Yanga dhidi ya Mbao msimu uliopita ni Deus Kaseke na Chirwa pamoja na Simon Msuva ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Morocco.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema Kamati ya Nidhamu ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Abas Tarimba, inatarajia kukutana wiki ijayo kwa ajili ya kujadili suala hilo.

“Yanga walikuwa na haki ya kulalamika maana kumekuwa na ukimya, lakini suala hilo litakwisha wiki ijayo baada ya Kamati kukaa na kuamua hatima yao,” alisema Lucas.

Kauli hiyo ya TFF imekuja siku moja baada ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa, kulilalamikia Shirikisho hilo kwa kukaa kimya juu ya suala hilo wakati wanajua wazi mchezaji huyo ni nguzo kubwa katika timu yao.

Alisema walipata barua kutoka TFF mwezi wa sita juu ya kusimamishwa kwa wachezaji hao, lakini hawakuainisha adhabu ambayo wanatakiwa kutumikia.

“Unajua barua hiyo ilisema kuwa wanatuhumiwa ila haikuwa na adhabu, hivyo tunaomba Kamati husika kukaa na kutoa mwongozo juu ya hilo, hata kama ni adhabu basi wapewe ili waweze kuitumikia kuliko sasa wanatumikia adhabu ambayo haipo.

“Chirwa ni mshambuliaji wetu tunamhudumia kila kitu, naye anahitaji kuitumikia ajira yake hivyo kukaa bila kujua hatima yake, inatuumiza sisi Yanga, hiyo ni hasara,” alisema Mkwasa.

Alisema pengo la mchezaji huyo katika timu yake linaonekana kwenye mchezo wao dhidi ya Simba na kama angekuwepo siku hiyo matokeo yangekuwa tofauti na waliyopata.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.