Ligi Kuu hiyoo, hatutarajii ubabaishaji

Dimba - - Jumapili -

MICHUANO ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza jana, ambapo takriban viwanja saba viliwaka moto wakati timu 14 zilipoumana na leo hii utapigwa mchezo mmoja pekee utakaowahusisha mabingwa watetetezi wa ligi hiyo, Yanga dhidi ya Lipuli ya Iringa.

Kwa kuwa historia inaonyesha michuano hii hutawaliwa na mizengwe ya mara kwa mara, ndiyo maana tunashauri mapema kuhusu umakini kwa timu zote zinazoshiriki pamoja na wadau wake.

Tunatambua kwamba ili timu ziweze kushiriki, basi wachezaji, viongozi, Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka nchini lazima wawe na ushirikiano ili kufanikisha michuano hiyo.

Hivyo basi, wadau hao pamoja na wapenzi na wanachama kwa pamoja, wanakuwa ndio wadau wanaofanikisha mambo yote, hivyo kuvurunda kwao kunaweza kukaifanya michuano isiwe na mvuto kama ilivyo kawaida.

Miongoni mwa mambo yanayokera wakati michuano hiyo ikiendelea, mara nyingi ni kuahirishwa kwa baadhi ya mechi ambapo matokeo yake kuleta usumbufu na pia kuzivurugia bajeti za timu zisizokuwa na udhamini wa kutosha.

Sisi Dimba tunatamani msimu huu suala la mechi kuahirishwa lisahaulie na iwe historia katika soka la Tanzania linalojipanga kupiga hatua kutoka hapa lilipo.

Kadhalika kumekuwapo na malalamiko mengi ya maamuzi, dhana ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikosa tiba ya kuiponya na hivyo kuendelea kutia dosari katika michuano hiyo mikubwa hapa nchini.

Dimba tunajua zipo changamoto nje ya uwezo wa mamlaka husika, kama vile uchakavu wa viwanja na miundombinu kwa jumla ambayo nayo imekuwa ikilalamikiwa, lakini inafahamika kwamba utatuzi wake unahitaji fedha nyingi zinazohitaji uwekezaji mkubwa zaidi.

Rai yetu inaangalia zaidi kupunguza malalamiko hayo tuliyoyaainisha hapo juu ambayo tunafahamu yapo ndani ya uwezo wa Bodi ya Ligi na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Tunaamini kuwepo kwa uongozi mpya wa TFF chini ya Rais Wales Karia na kamati yake ya utendaji, utakuwa na shauku kubwa ya kuanza kazi katika ligi yao ya kwanza, kwa kuifanya isiwe na migogoro kama zile zilizopita.

Kadhalika yapo mambo muhimu yanayohitajika hivi sasa ambayo yanaweza kusaidia kuboresha michuano hiyo, ambayo miongoni mwake ni kupatikana kwa ufadhili kwa klabu ili ziweze kushiriki vizuri na kuepuka kuwa wasindikizaji.

Uzoefu umetuonyesha kwamba, zipo timu nyingi zinazoshiriki ligi kuu zinazoonyesha kiwango kizuri mwanzoni na baadaye kuanza kulegalega kutokana na kuishiwa fedha na hivyo kushindwa kuhudumia wachezaji wake, matokeo yake hujikuta zikimaliza ligi kwa kupata matokeo mabaya.

Tunazitakia kila la heri timu zote zilizoanza jana kushiriki michuano ya ligi na hizi zitakazoanza hii leo, nia yetu ni kuona ligi inakuwa bora na kutoa timu ya Taifa nzuri itakayofanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.