Mabadiliko Uda Jazz 1980-83

Dimba - - Jumapili -

BILA shaka wadau wa ukurasa huu, mnakumbuka kwamba siku chache zijazo tutakuwa na mpambano mkali utakaokutanisha wanamuziki mashuhuri nchini dhidi ya kikosi kizima cha Msondo ngoma.

Nikukumbushe tu kwamba mtanange huo utapigwa Septemba 2, katika ukumbi wa Traverntine Magomeni, sasa tuendelee na mada hii.

Miongoni mwa bendi zilizokuwa zikivutia kwenda kupoteza mawazo kwa burudani ya muziki au kusikiliza aina ya magitaa na uimbaji wa aina yake na hata kukutana na mashabiki wanaojua muziki, ni katika maonyesho ya bendi ya Uda Jazz.

Ilikuwa ni bendi nzuri iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam, ndiyo maana kwa kifupi ikaitwa UDA.

Walipita wanamuziki wengi, achilia akina Beno Villa Antony, akina TX Moshi Wiliam, mchawi wa ridhim Fortunatus Kabeka, John Kijiko na wengine wengi, leo tunataka kuangalia mabadiliko ya miaka mitatu ya bendi hiyo.

Tunakumbuka kwamba baada ya kutamba kwa muda mrefu bendi hiyo ikiwa na vibao vyake kama vile Nachunga heshima, huku ikiwa chini ya mwamba wa upigaji solo, Hamza Kalala, hatimaye bendi hiyo ilimpoteza mwanamuziki huyo ambaye alirejea tena katika kundi lake la Vijana Jazz na hivyo akaiacha Uda ikiwa na magwiji wengine.

Ikapita katika mikono mingi lakini kwa bahati nzuri Kalala aliacha mwimbaji mzuri sana miaka hiyo ambaye pia alianza kuonyesha cheche zake, akijulikana kama Mikidadi Seif.

Kalala anaweza kujivunia kondakta huyo wa zamani wa UDA ambaye yeye alishiriki kuvumbua kipaji hasa pale alipomtaka ajaribu kazi hiyo wakati bendi ilipokuwa inapiga katika Ukumbi wa Wapiwapi uliokuwa eneo la Chang'ombe, Maduka Mawili ukilimikiwa na mfanyabiashara Khalfan Kikuyu.

Mikidadi ni kama vile aliokota dodo chini ya Mwarobaini kwani yeye alikuwa akipenda tu kuimba, huku akiendelea na kazi ya ukondakta, lakini siku

alipoambiwa anapata nafasi ya kuwa mwanamuziki na kutakiwa avue magwanda ya ukondakta, alifurahia kutimia kwa ndoto yake.

Hakuchukua muda mrefu kuaminiwa na kuachiwa kutunga na hili lilifanyika katika moja ya albam ambazo zilikuwa za kwanza baada ya Kalala kuiacha bendi hiyo.

Hiyo ilikuwa ni albam iliyorekodiwa Novemba 3, 1980 ambapo ndani yake kulikuwa na nyimbo nne ambazo tatu kati ya hizo alitunga Mikidadi.

Miongoni mwa nyimbo hizo ni moja tu iliyotungwa na mpiga magitaa mkali enzi hizo, feruz Kapalata ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa bendi ya Orchestra Super Matimila mwaka 1975.

Kapalata akaachia kibao kiitwacho Visa na vituko, kisha akamwacha Miky ambaye naye akaachia vitatu ambavyo ni Vick Acha Visa, Nenda Kaishi Salama na Tubole Tubowe aliouimba katika lugha ya Kimwela kutoka Mkoa wa Lindi.

Kwa mujibu wa Mikky, nyimbo hizo zilikuwa ni mfululizo wa matukio ya kweli ya kumsihi mwandani wake tokea hiyo ya kumtaka aache visa, lakini hakuelewa akaondoka ambako alimtakia akaishi salama, hadi pale alipomwambia Tubole tuboe yani rudi tulee.

Ufalme wa Mikky ulifanikishwa na wapiga magitaa mbalimbali, lakini katika tungo hizo gitaa la solo likacharazwa na John Kijiko, Solo namba 2 likatendewa haki na Feruz Kapata, huku mkali wa gitaa la kati ridhim aliyewahi pia kutesa na kundi la Afriso, Fornatus Kabeka akifanya vitu vyake.

Yusuf Juma na rafiki yake Athumani Soso hawa wakabadilishana kupiga gitaa zito la besi, huku Chipembele Said au Bob Chipe wakiungurumisha dram na tumba zikadhibitiwa na Mohamed Haroub.

Mikidadi alishirikiana kuimba na Christopher Mogela, Yusuf Mtambo bila kumsahau Kijiko ambaye naye pia alikuwa mtaalamu wa sauti, licha ya ukali wake katika gitaa la solo.

Hatimaye Ufalme wa kundi hili ukafikia tamati mwishoni mwa mwaka 1983, ambapo uongozi wa UDA uliamua kuiboresha bendi hiyo kwa kutwaa sura za vijana wa kisasa.

Katika mabadiliko hayo, mtaalamu wa magitaa aliyewahi kuandika historia ya kupanda ndege kwenda mjini Songea, Ijumaa kuwahi dansi la Jumamosi, Omar Makuka, akakabidhiwa mikoba ya kuiunda upya bendi hiyo.

Ujio wa Makuka enzi hizo akiishi Kinondoni ulikuja pia na baadhi ya sura mpya, ambapo kikosi sasa kilikuwa hivi, Juma Hoisen alikuwa akimsaidia kupiga gitaa la solo namba 2, akishirikiana na John Boaso, Charles KayokaRidhim, Athumani Soso na Juma Mohamed waliendelea kuwepo kikosini wakishirikiana kupiga gitaa la besi.

Safu ya upulizaji ilipewa watu makini enzi hizo wakiongozwa na mkali, Morgan Machege, akishirikiana na Ally Yahya na Hamisi Mnyupe ambao kwenye tamasha la Septemba 2, wataonekana wakifanya vitu vyao.

Mzee John Mbula aliendelea kutesa na Sax yake, huku Dram zikipigwa vizuri na Seif Said ambapo tumba ilibaki kwa Ahmed Katumba na kinanda kikipapaswa na John Bosco.

Waimbaji waliokuwa katika mabadiliko hayo ni pamoja na Fred Benjamin aliyekuwa akisifika pia pale alipokuwa na bendi ya Vijana Jazz, mwimbaji mwenye sauti nzito, Patrick Sheleta na mtaalamu mwingine mwenye sauti ya kinanda, George Mpupua.

Ukitaka kujua utamu wa sauti ya Mpupua, sikiliza wimbo wa Tofali la barafu au Mwanahawa wa Mwenge, Maisha kuvumilia na nilitaka iwe siri Vijana Jazz, na hapo UDA Sakina Kaharibu Masomo.

Wanaume hao waliingia Studio pale redio Tanzania Dar es Salaam, Januari 11, 1983 na kuachia vibao kama Sakina Kaharibu Masomo alioutunga Makuka, Kupenda ni Matatizo wa Juma Hosein,

Uchungu wa mwana, Makuka na Mpenzi ni wewe uliotungwa na Peter Thomas maarufu kama Sauti ya Simba.

Kwa taarifa tu bendi hiyo ilikuwa ni miongoni mwa bendi zilizokuwa na wanamuziki wanaojipenda kweli jukwaani na hata mitaani waliweza kuonekana wakiwa nadhifu na sare zao za suti zenye marembo ya drafti.

HAMZA KALALA MIKIDADI SEIF

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.