Ukimtaja Vieira mfikirie Robert Song

Dimba - - Jumapili - NA PRIVA ABIUD

Kule Brazil klabu ya Palmeiras ilikuwa na Patrick Vieira. Jina lake halisi ni Paulista. Huyu kijana baba yake aliuawa kwa bifu za madawa ya kulevya, huku yeye akiwa na mwezi mmoja tu. Baada ya kifo cha baba yake, alilelewa na baba wa kambo, Carlos ambaye naye alikimbizwa na wauzaji wa madawa ya kulevya na kuuawa. Kaka yake, Peterson ndiye aliyekuwa kama baba yake na alimlea katika maisha ya soka.

Zipo sababu nyingi sana za yeye kuitwa Vieira, kama sisi tunavyomuita Nadir Haroub Canavaro. Paulista akiwa na Miaka 16, alisajiliwa Sao Paolo kisha Palmeiras. Haikuwa kazi rahisi kwake kutoka katika maisha ya kuuza vyuma chakavu mpaka kupata mkataba wa miezi 6 pale Sao Paolo. Tuachane naye huyu.

Nchini Uswis, Mume wake Leonita Lekaj ndiye aliyeibuka kidedea mwaka 2011, kwa kuitoa Man United kwenye michuano ya Uefa akiwa na FC Basel. Huyu Vieira mpya wa Arsenal alipewa kadi nyekundu 3 kwenye msimu wa mwaka 2015/16 akiwa na Borussia M'bach. Ni mchezaji ambaye anaonekana sana kujiamini. Anafanya kile anachojisikia. Patrick Vieira wakati anambutua kiwiko Materrazi

alipoulizwa kwanini alifanya vile, alisema bila unafiki kuwa hampendi Materrazi. Ukiachilia mbali Richard Dunne kujifunga magoli (10), yeye na Patrick Vieira pamoja Duncan Ferguson ndio wanaongoza kwa kadi nyekundu EPL wakiwa na kadi 8 kila mmoja.

Granit Xhaka ambaye wengi wanaamini ndiye mrithi wa Vieira, mpaka sasa ana kadi nyekundu 2 ndani ya Arsenal akiwa amebakiza kadi 6 tu kuvunja rekodi ya Viera, lakini akiwa tayari ameshapewa kadi nyekundu 9 ndani ya miaka mitatu tu uwanjani akiwa na miaka 24.

Kadi walizopewa akina Duncan na Vieira kwa miaka 10 na zaidi, mdogo wao Xhaka tayari anazo na zaidi kwa miaka mitatu tu. Hapendagi ujinga.

Licha ya kuwa na rekodi mbaya lakini bado anaonekana kuwa ni mpambanaji sahihi kwenye dimba la katikati. Wakati Granit Xhaka anavutwa jezi na Pogba hakujali sana, kwa sababu mwaka 1986, mlango wa nyumba yao uligongwa. Mwaka huo walikuwa wakiishi Kosovo, Jimbo la huko Yugoslavia. Baba yake mzee Rajip Xhaka alitoka kufungua mlango. Ghafla alikutana na polisi waliomvuta shati lake na kumtoa nje kama Pogba alivyofanya kwa kumvuta jezi yake. Baba yake alikuwa mbishi sana, kitendo kilichowakera sana polisi. Xhaka amekuwa mkorofi sana akiwa katika dimba la kati, kitendo kilichomkera hata Pogba. Xhaka aliwahi kusema hawezi kuacha mpira wa kukaba kwa nguvu na kucheza takoling sana. Ndio asili yake. Baba yake hakuwahi kumwonea mtu aibu.

Ukorofi wa mzazi wake ulimfanya afungwe gerezani kwa miaka mitatu kwa kile kilichoitwa kuwa aliihujumu Serikali iliyokuwa madarakani. Nani ambaye hakumbuki tifua tifua la Vieira na Roy Keane? Basi kama hukumbuki hata hili mbungi la Xhaka na Pogba hukuliona?

Licha ya Xhaka kuanza msimu vibaya, baada ya Arsene Wenger kubadili mfumo, nani hakuona kazi ya Xhaka? Wenger aliamua kuachana na mfumo wa 4 4 2 na kuhamia mfumo wa 3 4 2 1, ni maamuzi magumu kuwahi kutokea chini ya ardhi, hii ni sawa na kutukana wajeda. Hii ni baada ya Wenger kugundua udhaifu wa Xhaka. Alifahamu Xhaka ni nani, alikumbuka alivyokuwa akiteseka kwa Vieira. Ndio alibadilisha mfumo ili kumpa xhaka uhuru zaidi.

Kwa mfano mwepesi tu wakati msimu unaanza Xhaka alikuwa na asilimia 61 ya pasi zilizokamilika kwenye mfumo wa 4 4 2. Rekodi mbovu kabisa kwa mchezaji wa timu inayocheza pasi nyingi kama Arsenal. Mfumo huo ulimfanya kuwa mkabaji zaidi, jukumu ambalo si lake. Lakini kwenye mfumo wa 3 4 2 1 ambapo Chamberlain na Coqulien walimsaidia kukaba, alikuwa na ustadi wa pasi uliofikia asilimia 81. Ndio .... Wenger hapa alilamba joka na alijiamini. Kwani wewe hukuona alitwaa FA mbele ya Mabingwa Chelsea?

Miezi minne ya awali Xhaka alitengeneza nafasi 10 kwenye mfumo ule ule wa 4 4 2, ovyo kabisa, hapa tunasema mtoto alitumwa mafuta ya taa akanunua ya kula, je hayo mafuta utapeleka wapi wakati yamewekwa kwenye chupa ya mafuta ya taa? lakini kwenye mfumo wa 3 4 2 1 alitengeneza nafasi 25, pia alitengeneza magoli mawili kwenye mfumo huu 3 4 2 1 ilhali hapo awali kwenye 4 4 2 hakutengeneza goli lolote.

Hata Vieira mwenyewe akiwa kocha pale kwenye Uwanja wa Yankee Stadium, aliamua kubadili mfumo na kuanza na mfumo wa 3 4 3 na klabu yake ya NewYork City.

Baada ya Wenger kugundua Vieira hawezi kuhimili presha za kucheza kama kiungo mkabaji, nyuma yake alimweka Gilbeto au Parlour. Hivyo ameamua kumweka Xhaka na Coquelin nyuma yake huku pemben akaamua kuweka mabeki watakaomfanya Xhaka asihagaike sana.

Tukirudi nyuma kidogo Mzee Ragip Xhaka akiwa na miaka 22, akisoma Chuo Kikuu cha Pristina, alikuwa hana uhuru ndani ya nchi yake kwa kile kilichodaiwa alijikuta Tundu Lissu/Lema. Baba yake Xhaka alikuwa mtukutu, hakuwa muoga, alikuwa mpambanaji na huenda naye huko kwao alimuita raisi wao Dikteta Uchwara. Xhaka ameiga maisha ya baba yake, haogopi kadi, amempa Wenger Presha kubwa kiasi cha kubadili mfumo. Wenger ni mwoga, asingeweza kuweka Euro 35 benchi kwa sababu ya kadi nyekundu, imembidi amwekee wakabaji wengine mbavu za pembeni ili kazi yake iwe kuchezesha timu. Tunasema ni kama mikutano ya siasa imekatazwa, Xhaka anapaswa kuwa jimboni mwake tu (katikatiki ya uwanja). Binafsi namuona Vieira amerudi, lakini amerudi na rangi nyingine. Hata asipopata mafanikio ya Vieira lakini uwezo wake kila mtu ameuona.

Robert Song

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.