Majambazi yavamia DRFA, yapora fedha na baadhi ya vitu

Dimba - - Jumatano - NA SALMA MPELI

WATU sita wanaosadikika kuwa ni majambazi, jana asubuhi walivamia katika ofisi za Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kupora fedha, simu za mkononi kadhaa pamoja na kompyuta aina ya Laptop.

Akizungumza na wanahabari jana, Katibu Mkuu wa DRFA, Kanuti Daudi, alisema aliingia ofisini hapo saa 4:25 na kukutana na mmoja akiwa amekaa mapokezi aliyetaka kujua kama yeye ndiye Kanuti.

Alisema alipoitikia kuwa ni yeye, alimchukua na kumtaka wapande juu ziliko ofisi zao na kumwambia asipige kelele, huku akimuamrisha kufanya kile alichokuwa akikitaka.

"Ilikuwa kama sinema vile kwani nilipoingia tu mapokezi, nikakutana na huyo mtu na kunitaka nipande juu kimyakimya bila kupiga kelele na nilipofika huko nikakuta wenzangu wengine wamefungwa kamba na mimi nikafungwa pia," alisema.

Aliongeza kuwa, baada ya hapo walimtaka kutoa pesa ambazo walidai zipo ofisini hapo kiasi cha Sh milioni 150, kitu ambacho alikanusha kuwepo kwa fedha hizo ofisini hapo.

Kanuti alisema watu hao walichukua funguo alizokuwa nazo mfukoni mwake na kuondoka nazo, lakini kabla ya hapo waliweza kuondoka na simu, pesa alizokuwa nazo kiasi cha laki mbili, mtu mwingine alikuwa na laki saba, mwingine tena laki mbili na fedha nyingine laki nne na nusu ambazo zilikuwa ofisini hapo.

"Waliweza kuchukua fedha kiasi fulani kutoka kwangu na kwa wafanyakazi wengine hapo, walichukua simu zetu pia na laptop, baadaye waliondoka zao," alisema Kanuti.

Kanuti alilishukuru Jeshi la Polisi kuwahi kufika kutoa msaada eneo la tukio japo walikuta watu hao wameshaondoka, lakini hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo ila tu kupoteza baadhi ya vitu pamoja na fedha hizo ambazo idadi kamili haijajulikana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.