Bartomeu ameitusi La Masia na kutufumbua kitu

Dimba - - Jumatano -

IKI iliyopita ndani ya kolamu hii niliandika jinsi watu wanavyotakiwa kuiheshimu Real Madrid na kocha wao, Zinedine Zidane. Ndani ya andiko lile nilisema Barca inapitia kwenye kipindi kigumu katika maisha yao.

Wiki hii nimekuja na Barca wenyewe waliovurugwa. Leo nitayaelezea mambo matatu yaliyowavuruga. Jambo la kwanza ni Neymar Santos, jambo la pili ni Ousmane Dembele na jambo la mwisho ni Josep Mario Bartomeu.

Haya ni mambo yaliyoifikisha hapa Barca. Muda huu ambao Lionel Messi amepungua kasi kutokana na jua la utosi kumgonga utosini na Barca ilimtegemea Neymar kuwa ndiyo mrithi wake.

Barca ilimuweka Neymar katika mizani hiyo, ndiyo maana kila alichokitaka alipewa, kasoro ufalme ambao bado ulikuwa mikononi mwa Messi.

Kitendo cha Neymar kutimka ilikuwa lazima kiwaache mdomo wazi watu wa Barca, hasa wakati huu ambao nyumba ya jirani (Madrid) inaimarika siku hadi siku.

Mashabiki wa Barca wamekasirika. Wamemjia juu rais wao, Bartomeu, wanataka ajiuzulu. Ikiwezekana arudi Juan Laporta, rais aliyewapa heshima ya kulitawala soka la Ulaya. Ndani ya timu kuna vurugu, hakuna maelewano.

Mashabiki wamejiaminisha mtu pekee anayeweza kuwaokoa kwenye mikono hii ya Bartomeu waliyoiita mikono ya shetani ni Laporta, aliyemaliza muda wake.

Lakini katiba ya Barca inasimama na Bartomeu, ambaye hana mtazamo mzuri mbele ya wanachama (mashabiki) wake wanaomuona mlafi wa fedha kwa kukubali kusaini hundi ya mauzo ya Neymar.

Sababu ya pili iliyokuja kuvuruga mambo ni usajili wa Dembele. Barca imetoa kiasi kikubwa cha fedha kulinunua kinda hilo. Moja ya sera za Laporta ilikuwa ni kuwaamini vijana wanaotengenezwa chuoni hapo La Masia.

Muda mrefu wa utawala wa Laporta, Barca haikuwahi hata kukaribia kutoa Pauni milioni 60 kumsajili mchezaji. Xavi Hernandez, Andres Iniesta, Messi, Gerrard Pique na wengineo walitosha kuifanya Barca iwe kwenye kilele, kwanini hili linashindikana kipindi cha Bartomeu?

Kingine kilichowatia kichefuchefu mashabiki hao ni rangi ya Dembele. Barca ni moja ya timu yenye ubaguzi wa rangi. Sitaki kukumbuka walichokutana nacho Yaya Toure, Alex Song na Seydou Keita. Sitaki kukumbuka.

Kama Samuel Etoo aliyekuwa akifunga idadi kubwa ya mabao klabuni bado alibaguliwa na rangi yake, vipi hawa wakina Toure ambao nafasi zao ni kulinda mabao na si kufunga mabao yenyewe?

Kitendo cha kusainiwa hundi ya kiasi kikubwa cha fedha kumsajili mtu mweusi ni kibao cha kelbu kwa mashabiki hao wenye chuki na watu weusi.

Mashabiki Barca walimtaka Philipe Countinho, ndiyo maana kila kukicha waliongeza presha kwa uongozi wao wa juu kumsajili, lakini kitendo cha dili hilo kutokamilika mpaka sasa, lakini kukiwa na taarifa dili hiyo itakamalika baadaye, imewaudhi mashabiki wa Barca.

Nataraji kuiona Barca yenye vipande vipande msimu huu. Haitakuwa Barca iliyotulia na kucheza soka la kitabuni na kila mmoja kuitamani.

Jambo la pili ni usajili wa Dembele kuwarudisha mbali mashabiki hao ambao wanaikumbuka kauli iliyowahi kutolewa na aliyekuwa kocha wao, Pep Guardiola, kuhusu kumsajili Jack Wilshere msimu wa 2010/11.

Msimu huo Barca walikutana na Arsenal katika hatua ya 16 ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na Wilshere kupiga mpira mwingi na baada ya mchezo kwisha Pep aliulizwa na waandishi wa habari vipi siku moja anatamani Wilshere acheze Barca chini yake?

Pep alilisikiliza swali hilo kwa umakini, akashusha pumzi, kisha akamjibu mwandishi ìChuoni kwetu (La Masia) kuna Wilshere 100 ambao hawajapata nafasi, hivyo ni ngumu kutoa kiasi chochote kumsajili yeye (Wilshere)î. Jibu hili liliwafurahisha mashabiki wa Barca, wanaoamini kila kitu kizuri kinapatikana kwao.

Jambo la tatu ni kitendo cha Bartomeu kumsajili Dembele, ni kama ameitusi La Masia, ambayo ukweli wa mambo hivi sasa haizalishi tena nyota mahiri. Huu ni ukweli mchungu ambao ni mgumu kumezwa na mashabiki Barca.

La Masia ya leo haina tena ubavu wa kuwazalisha wakina Xavi, Messi. Inazalisha wachezaji wazuri wenye viwango vya kawaida. Katika ukweli wa hili, ni lazima Bartomeu afanye hiki anachokifanya sasa.

Dunia ya soka leo inanuka fedha. Kwa anachokifanya Bartomeu wakati huu, kinahitaji maono kumwelewa na si kumwaga povu.

BATROMEU INIESTA

XAVI MESSI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.