HONDO WA MECHI ZA UFUNGUZI VPL 2017/18

Dimba - - Jumatano - NA MAREGES NYAMAKA vizuri kwa

SIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania umeanza kurindima katika viwanja mbalimbali nchini, tayari mechi za mzunguko wa kwanza zimepigwa na kila timu imevuna ilichopanda.

Simba, iliyotumia zaidi ya Sh bilioni 1.3 kufanya usajili, ilianza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuikamua Ruvu Shooting mabao 7-0, Prisons ikaicharaza Njombe Mji mabao 2-1, Singida United ikapigwa mabao 2-1 na Mwadui FC, huku Azam ikimaliza uteja kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda.

Mbeya City, ambayo ilikuwa haijawahi kuanza na ushindi katika mechi yake yoyote ya kwanza tangu ilipopanda daraja msimu wa 2013/2014, ilitoa gundu baada ya kuanza kwa kicheko msimu huu, kwa kuipa Majimaji kichapo cha bao 1-0, wakati Kagera Sugar ikianza vibaya kwa kufungwa bao 1-0 na Mbao FC ya Mwanza.

Mtibwa Sugar pia ilianza kuibugiza Stand United bao 1-0.

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ulikamilika Jumapili kwa bingwa mtetezi, Yanga, kubanwa mbavu na timu iliyopanda daraja ya Lipuli FC na kutoka nayo sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kwa ujumla mabao 19 yalifungwa katika mechi saba za mzunguko wa kwanza zilizochezwa Jumamosi na Jumapili, huku Emmanuel Okwi wa Simba akiweka rekodi kwa kufunga mabao manne peke yake katika mechi moja.

Ligi ya msimu huu imeonekana wazi kuwa itakuwa na ushindani kutokana na usajili uliofanywa na klabu hizo. Mbali na Simba kuvunja benki ili kujenga kikosi madhubuti, Singida United, Yanga pia zimetumia fedha nyingi kuimarisha vikosi vyao. Yote tisa, kumi ni kwamba, kuna mambo ambayo hayana budi kufanyiwa kazi kikamilifu ili kuepusha malalamiko na kuhakikisha mwisho wa msimu bingwa anapatikana kwa haki.

Makala hii inakuletea matukio kadhaa na takwimu za michezo yote ya awali.

Weka pembeni ushindi wao mnono ulionogeshwa na mshambuliaji wao mahiri Mganda, Emmanuel Okwi kwa kuingia wavuni mara nne katika ushindi wa 7-0, kubwa ni timu hiyo kuwa na mwendelezo wa kushinda mechi zake za kwanza za ligi, ambapo ushindi huo unawafanya kushinda mara ya 10 mfululizo.

Takwimu zinaonyesha mnyama alipoteza mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi msimu wa 2007/2008, alipopoteza ugenini kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, mtanange uliopigwa katika dimba la Mkwakwani, Tanga. Timu ya Simba imeendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza mechi zake za ufunguzi wa Ligi Kuu kwa msimu wa 10 sasa. Mara nyingi imekuwa ikishinda na mara chache sana kutoka sare.

Mara ya mwisho timu hiyo kufungwa mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu, ilikuwa msimu wa 2007/08, ilipochapwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga, kwa bao la Sunday Peter, dakika ya 44.

Ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting umeifanya timu ya Simba kufunga magoli mengi siku ya ufunguzi tangu 2008.

Mara ya mwisho timu hiyo kushinda magoli mengi mechi ya ufunguzi ilikuwa ni Agosti 22, 2008, Ligi Kuu msimu wa 2008/09.

Iliichapa Villa Squad mabao 4-1 jijini Dar es Salaam. Yalikuwa ni magoli ya Emeh Izuchukwu aliyefunga mawili, Mussa Hassan Mgosi na Ramadhani Chombo ëRedondoí, goli la kufutia machozi la Villa Squad likifungwa na Mathew Chesido.

Neno la wachezaji wazoefu katika soka limekuwa na maana kubwa kutokana na jinsi wanavyoweza kuzisaidia timu zao kupata matokeo chanya, kama ilivyotokea kwa timu za Mwadui FC ya mkoani Shinyanga na Mbeya City kupata matokeo bora mbele ya wageni wa ligi hiyo.

Mwadui iliweza kuiangushia Singida United, inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Hans Van Pluijm, kipigo cha mabao 2-1.

Kilichoonekana katika mtanange huo ni uzoefu wa wachezaji nyota wa Mwadui, akina Malika Ndeule, Hassan Kabunda na wengineo, tofauti na Singida United, ambayo licha ya kuwa na wachezaji wenye majina na wa daraja la juu, lakini mazingira ya kutozoeana kitimu pamoja na aina ya soka la wapinzani wao, vilionekana kuwa kikwazo kwao.

Dhahama kama hiyo pia iliwakumba wageni wengine wa ligi, timu ya Njombe Mji, iliyo chini ya kocha Hassan Banyai, ambayo ilikaribishwa katika ligi kwa kukubali kufungwa mabao 2-0 na Tanzania Prisons, ambayo haijaondokewa na wachezaji wake wengi.

Hata hivyo, benchi la ufundi na viongozi wa Njombe Mji wameonekana kulilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na kutofikishiwa kwa wakati leseni za wachezaji, ambapo wachezaji watano waliokuwa kwenye mipango ya kocha ilibidi wawe watazamaji jukwaani, kutokana na kutokuwa na leseni hadi mpira unaanza.

Malalamiko kama hayo pia yametoka kwa timu za Ndanda FC na Kagera Sugar, ambazo pia zimeathirika kwa kiasi.

Wawili hao, Njombe Mji na Singida United, walikuwa tofauti na mgeni mwenzao, Lipuli FC ya mkoani Iringa, ambayo ilifanikiwa kupata pointi moja ugenini dhidi ya bingwa mtetezi, Yanga.

Hiyo ilitokana na kikosi chao kuwa na asilimia 90 ya wachezaji ambao ni wazoefu katika ligi, jambo ambalo lilimrahisishia kocha Seleman Matola kufanya kazi yake ya kupata matokeo kuwa nyepesi.

Miongoni mwa wachezaji hao walioonekana kuwa ngangari na kuwazuia nyota wa Yanga ni pamoja na Paul Ngalema, Malimi Busungu, Omega Seme na nahodha Mghana, Asante Kwasi.

Jumla ya mabao 19 yaliyofungwa mechi hizo za awali yameweka rekodi, kwani ni mabao mengi zaidi katika misimu ya huko nyuma, ikiwamo misimu miwili iliyopita, ambapo 2016/17 yalifungwa mabao 13 pekee, huku msimu wa 2015/16 makipa wakiokoteshwa mipira wavuni mara 12.

Idadi hiyo ya mabao imechagizwa zaidi na ushindi wa Simba wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, kama ilivyowahi kuwatokea kwa Yanga kuwapa kipigo kama hicho maafande hao katika mechi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo msimu wa 2013/14. Azam, Mbao zatusua

Ni timu mbili pekee zilizopata ushindi ugenini, licha ya mara nyingi makocha wengi kuwahamasisha na kuwaelekeza wachezaji wao kama uwanja wa nyumbani ndipo mahali panapotakiwa kukusanya pointi nyingi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo sapoti ya mashabiki.

Lakini hilo lilionekana kwenda kombo kwa timu za Kagera Sugar ya Bukoba, iliyoshindwa kuutumia vyema uwanja wake wa Kaitaba, baada ya kufungwa na Mbao bao 1-0, huku Ndanda ya Mtwara ikichemsha uwanjani Nangandwa Sijaona kwa kubamizwa idadi kama hiyo na timu za Azam FC.

Azam ilifanikiwa kuibuka na ushindi huo dhidi ya Ndanda katika dimba la Nangwanda, ambalo mara kadhaa huko nyuma ilikuwa ngumu kupata matokeo bora, ambapo tangu wanakuchele hao wapande daraja, matajiri wa bongo walikuwa wameshinda mchezo mmoja pekee katika viunga hivyo.

Mbao ni kama walilipiza kisasi cha msimu uliopita, walipofungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, ukiwa ni mchezo wa 29, kuelekea ligi kufika tamati.

Wapigadebe hawa wameendeleza unyonge wao wa kutoonja ladha ya ushindi katika mechi za ufunguzi tangu ilipopanda ligi msimu wa 2014/2015, baada ya kuambulia kichapo cha bao 1-0 ugenini katika dimba la Manungu Complex, dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Takwimu zinaonyesha msimu uliopita walitoka suluhu na majirani zao, Mbao FC, huku msimu wao wa kwanza kucheza ligi hiyo 2015/16 ilipoteza mechi kwa kufungwa bao 4-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara.

Rekodi nyingine imewekwa na Mbeya City, baada ya kushinda kwa mara ya kwanza mechi ya ufunguzi tangu ipande Ligi Kuu msimu wa 2013/14. Ilitoa gundu kwa kuichapa Majimaji bao 1-0.

Msimu huo wa kwanza wa ligi ikiwa nyumbani Sokoine, ilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar, ikatoka tena suluhu nyumbani dhidi ya JKT Ruvu msimu wa 2014/15, ikachapwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar mechi ya ufunguzi msimu wa 2015/16.

Msimu uliopita 2016/17 ilianzia ugenini dhidi ya Kagera Sugar na kutoka sare ya bila kufungana.

Wachezaji wa Simba wakishangilia

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.