Tshishimbi anapotukumbusha vitu vya Hamisi Gaga 'Gagarino'

Dimba - - Jumatano -

KUNA mambo mengi yamepita katika historia ya soka ya Tanzania, lakini kuna baadhi ambayo ni vigumu kuyasahau na huenda yakabaki kuwa gumzo kwa kipindi kirefu sana.

Katika historia ya Tanzania, wako viungo wengi sana wamepita lakini jina la Hamis Thobias Gaga 'Gagarino,' kamwe halitosahaulika.

Huyu alikuwa ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga, kutoa pasi zenye macho na hata kufunga mabao na kwa kiasi kikubwa alimiliki vilivyo dimba la kati, liwe la juu ama la chini.

Kiungo nyota wa klabu ya Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyesajiliwa na timu hiyo msimu huu, siku ya Jumatano, wiki iliyopita, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliokutanisha timu yake dhidi ya Simba, alionesha vitu adimu ambavyo vilikuwa vikioneshwa na 'Gagarino.'

Tshishimbi, ambaye katika mchezo huo wa Jumatano iliyopita, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam alipangwa kiungo mkabaji namba sita, lakini alikuwa akihaha karibu nusu nzima ya uwanja na kuonesha vitu adimu, huku akisaidiana na kiungo mshambuliaji, Thaban Kamusoko.

Katika mchezo huo, ambao kiufundi ulionekana kulingana, Tshishimbi alionekana kutakata mno na kucheza vyema, huku akiwalisha washambuliaji wake kwa pasi za uhakika, Donald Ngoma, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin.

Katika mchezo huo, ambao ulivuta hisia ya wapenzi, mashabiki wengi waliohudhuria mechi hiyo, Tshishimbi alionekana kumudu vyema majukumu yake katika namba yake ya kiungo mkabaji, huku akicheza soka la uhakika..

Pia katika mchezo huo, nyota huyo ambaye anaonekana kuziba kiu ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo, alipokuwa na mpira ilikuwa ni vigumu kwa mchezaji mwingine yeyote kumnyangíanya, hali ambayo kwa kiasi fulani wachezaji wa timu ya Simba walikuwa wakimchezea rafu.

Pamoja na kiwango chake cha juu alichoonesha uwanjani, Tshishimbi pia alikuwa ni mmoja wa waliofunga penalti zao kwa upande wa Yanga wakati wa changamoto ya mikwaju hiyo, baada ya timu hizo kutoka suluhu ndani ya dakika 90 za kawaida.

Kutokana na kiungo huyoalivyokuwa akicheza katika mchezo huo kwa umahiri mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga za maudhi na kujaribu kupiga mashuti, alionekana dhahiri kwa wapenzi wa soka kuwa alikuwa akicheza sawasawa na kiungo wa zamani, Hamis Thobias ëGagarinoí.

Wakati wa enzi zake za kucheza soka miaka ya 1980 mwishoni na 1990 mwanzoni, Gaga akichezea klabu ya Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, alikuwa akisifika mno kwa kucheza kandanda la uhakika katika nafasi za kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji.

Licha ya Gaga kuwa na umahiri mkubwa wa kumudu kucheza vyema nafasi hizo mbili za kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, pia fundi huyu alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingine nyingi kama beki wa kati nne, tano na mshambuliaji namba 10.

Gaga alimudu kucheza vyema nafasi zote hizo kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga za maudhi, nguvu pale inapohitajika, mashuti makali na hivyo kuwapa kazi ya ziada makipa wa timu pinzani kudaka michomo yake.

Mbali na sifa zote hizo alizokuwa nazo, pia Gaga alikuwa mtaalamu wa kupiga mipira ya adhabu ndogo na kubwa, akiwamo mipira ya penalti kama inavyoonekana hivi sasa kwa Tshishimbi na ilikuwa si rahisi kukosa kufunga penalti.

Kutokana na umahiri mkubwa aliokuwa nao wa kucheza vizuri awapo uwanjani, ilikuwa ni nadra sana kutopangwa katika kikosi cha kwanza.

Alipokuwa akichezea klabu ya Simba alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa kutegemewa na hata alipojiunga na Yanga mwaka 1993 pia alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa kutegemewa, japokuwa ilitokea wakati alikuwa akipokezana na kiungo Steven Mussa, kwani naye alikuwa mtaalamu mno.

Hivi sasa hatunaye tena fundi Gagarino, kwani alifariki dunia mwaka 1996. Hivyo kwa uchezaji wake hauna tofauti kabisa na uchezaji wa kiungo mkabaji Tshishimbi, ambaye hivi sasa ameanza kujizolea umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa soka nchini, hususan wa klabu yake ya Yanga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.