TSHISHIMBI AISHI KIFALME DAR

Dimba - - Jumatano - NA CLARA ALPHONCE

KIUNGO mpya wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo -DRC, ni kama mfalme ndani ya kikosi cha timu hiyo. Amekuwa staa wa timu kwa muda mfupi na maisha yake yanakwenda kifalme.

Tshishimbi alitoka kwao Congo-DRC akiwa mchezaji asiye na umaarufu mkubwa, lakini mwenye kipaji cha hali ya juu na chenye mvuto.

Lakini kutokana na ubora aliouonyesha katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba, ameweza kuwashawishi kwa kiasi kikubwa mashabiki wa timu hiyo akiwemo tajiri mmoja mmoja ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji, kiasi cha kumpa vitu ambavyo vimemfanya mchezaji huyo kuishi kama mfalme hapa nchini.

Tshishimbi ni mmoja wa wachezaji waliosajiliwa na Yanga msimu huu akitokea katika klabu ya Mbabane FC ya nchini Swaziland.

Kiungo huyo mwenye mambo mengi uwanjani, tangu atue nchini amekuwa akipewa huduma ya kipekee na tajiri huyo, tofauti na wachezaji wengine na inasemekana kuwa hata pesa ya usajili wake ametoa kigogo huyo.

Mbali na kupewa magari ya kifahari kutembelea, pia amempa nyumba ya kifahari ya kuishi yenye kila kitu (Apartment) na ambayo ni tofauti na zile wanazokaa nyota wengine wa kigeni, akina Dolnad Ngoma, Obrey Chirwa na Thaban Kamusoko.

Nyumba aliyopewa kuishi Tshishimbi iko maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, sehemu wanakokaa matajiri na inamilikiwa na kigogo huyo wa Yanga.

Pamoja na kwamba Chirwa ndiye ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi katika Ligi Kuu ya Tanzania, baada ya kununuliwa kwa Sh milioni 200 msimu uliopita, lakini hakuwahi kuishi maisha ambayo anaishi Tshishimbi.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa Yanga ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, aliliambia DIMBA Jumatano kuwa, kigogo huyo amempa nyumba mchezaji huyo ili aweze kumfanya kuishi mazingira mazuri na kucheza soka bila bughudha.

"Tajiri ndio kaamua bwana lolote analotaka kufanya juu ya Tshishimbi anafanya hakuna wa kumzuia, hata hivyo aliamua kumpa nyumba kwa kuwa hakutaka mchezaji huyo akae hotelini.

"Pia amekuwa akimbadilishia magari anavyojisikia, kwa ajili ya kwenda nayo mazoezini na kutembelea katika 'misele' ya kawaida, siku anakuja na Ranger Rover, saizi kampa Ford Ranger," alisema Kiongozi huyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na Tshishimbi kukaa Mbezi Beach kwa sasa, lakini bado wana mpango wa kumtafutia 'Apartment' nyingine nzuri zaidi katikati ya jiji atakakoishi na wenzake wa kigeni wanaoishi maeneo ya Shekilango kwa sasa, ili iwe rahisi kwao kufikika pindi watakapohitajika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema ni kweli Yanga wamempangia nyumba mchezaji huyo kwa tajiri huyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.