Okwi abebeshwa mabomu ya kuiua Misri

Dimba - - Jumatano - NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 7-0, Simba walioupata dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baadhi ya mashabiki nchini Uganda wamempa neno straika wao, Emmanuel Okwi.

Mashabiki hao wamemtaka Okwi kuifungia idadi kama hiyo ya mabao timu yao ya Taifa ya Uganda ‘The Crane’ itakapowakabili Misri kesho katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, itakayofanyika mwakani nchini.

Mchezo huo ambao utachezwa kesho Uwanja wa Namboole nchini humo, unatarajiwa kuwa mkali kutokana na kila timu kutaka kupata ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu michuano hiyo, ambapo Okwi ni kama ametwishwa zigo kubwa la kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Baada ya mchezo huo dhidi ya Ruvu Shooting kumalizika, mwandishi mwandamizi wa mtandao maarufu nchini Uganda, Kawowo Sport anayeitwa David Isabirye, alitumia mtandao wake wa kijamii wa Facebook kuwafikishia ujumbe kuwa Okwi amefunga mabao manne ndipo mashabiki hao wakaanza kufunguka.

Wa kwanza kuposti ujumbe wake katika mtandao huo wa Facebook wa mwandishi huyo, ni Nyakana Peter ambaye aliandika kwamba wanamtaka Okwi kufunga mabao kama hayo dhidi ya Waarabu hao kutoka nchini Misri.

Nyakana aliandika: "Tunayataka mabao hayo kwenye mchezo wetu dhidi ya Misri," alisema, maneno ambayo yanafanana na mwenzake Glen Marcus Kats, huku Kelechi Esli David akishangaa kwamba Okwi amerudi kujiunga na Simba kwani alidhani bado yupo Ulaya akikipiga huko.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.