CANAVARO AMPA MBINU TSHISHIMBI

Dimba - - Jumatano - NA JESSCA NANGAWE

BEKI wa Yanga, Nadir Haroub ‘Canavaro’, amempa mbinu kiungo mpya wa Yanga, Pappy Tshishimbi na kumtaka kutotishwa na wanaompania kwenye ligi kuu kwa kuwa ni sehemu ya changamoto za wachezaji wanaofanya vyema.

Tshishimbi ameonekana kupaniwa na wachezaji wa ligi kuu kutokana na kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliowakutanisha na mahasimu wao Simba.

Tshishimbi raia wa Congo ametua Jangwani na kuonekana kukata kiu ya sehemu ya kiungo kutokana na kucheza vyema, huku akionekana kukabili vyema nafasi hiyo muhimu.

Akizungumza na DIMBA, Canavaro alisema kiungo huyo anapaswa kukabiliana na changamoto anazokutana nazo na kufanya majukumu yake kama mchezaji ili kuisaidia timu yake ifanye vizuri.

“Aaah yeye ni mchezaji na atambue wajibu wake tu, kikubwa alinde kipaji chake na atambue ni kawaida kwa mchezaji mwenye uwezo kukabiliana na changamoto kama hizo, namshauri tu apambane na hilo ili kutimiza ndoto zake za kucheza,” alisema Canavaro.

Beki huyo aliongeza kuwa wako kwenye mikakati ya kuhakikisha wanatetea ubingwa wao kwa mara nyingine kwa kuhakikisha wanashinda katika michezo ya mapema ili kupigia hesabu za ubingwa mapema.

Yanga ambayo ilitoka sare ya 1-1 na Lipuli FC, itakutana ugenini na Njombe Mji katika mchezo unaokuja, ikiwa ni mwendelezo wa mechi zake za Ligi Kuu Tanzania bara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.