Samatta atua Stars, Msuva kuwasili leo usiku

Dimba - - Jumatano - NA SALMA MPELI

NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amewasili alfajiri ya jana na kujiunga na wenzake katika kikosi cha timu hiyo kilichoingia kambini tangu juzi jioni, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Stars wanatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru, kucheza na timu ya Taifa ya Botswana, mchezo wa kirafiki unaotambuliwa na Fifa.

Akizungumza na DIMBA jana, Meneja wa Stars, Daniel Msangi, alisema mchezaji huyo aliingia nchini jana alfajiri lakini hakuweza kujiunga na wenzake katika mazoezi ya jana asubuhi kutokana na uchovu.

Alisema wachezaji wengine kama Msuva anatarajiwa kuwasili usiku wa leo, kwani juzi alichelewa ndege na hivyo kulazimika kuanza safari jana.

“Wachezaji wote wameshawasili hasa wale wanaocheza ligi ya ndani, lakini wa nje ambao tayari wamefika ni Elius Maguli na Mbwana Samatta, huku Msuva tukimtarajia kesho (leo) usiku,” alisema.

Alisema wengine ni Abdi Banda ambaye alitarajiwa kuwasili jana jioni na Khamis Abdallah wa Kenya ambaye aliwasili jana mchana, huku Farid Mussa akitarajiwa kuwasili leo pia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.